London, England
Bilionea wa Marekani mwenye asili ya Iran, Jahm Najafi (pichani) inadaiwa ametenga kitita cha Pauni 3.7 bilioni kwa ajili ya kuinunua klabu ya Tottenham Hotspur.
Najafi ambaye ni mwenyekiti wa kampuni ya uwekezaji katika michezo ya MSP Capital, si jina geni kwenye michezo, ni mmoja wa watu wenye hisa katika timu ya mpira wa kikapu ya Phoenix Suns.
Bilionea huyo mmiliki wa makampuni ya Najafi, inadaiwa amepanga kufanya kikao na mmiliki wa Spurs, Joe Lewis pamoja na mwenyekiti wa klabu hiyo Daniel Levy.
Vyombo mbalimbali vya habari jana na leo Jumatano vimeripoti habari hiyo ingawa viongozi wa klabu hiyo hawajawa tayari kusema lolote kuhusu kuwapo kwa mpango huo.
Spurs kwa msimu huu imefuzu kushiriki hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na tayari imepoteza mechi ya kwanza jana Jumanne kwa kuchapwa bao 1-0 na AC Milan ya Italia.
Katika Ligi Kuu England (EPL), timu hiyo inayonolewa na kocha Mtaliano, Antonio Conte inashika nafasi ya tano na inapambana kumaliza msimu katika Top Four.
Spurs inamiliki uwanja wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 63,000 ambao ndio uwanja wao wa nyumbani ambao walitumia kiasi cha Pauni 1 bilioni kuujenga.
Iwapo mpango huo utafanikiwa Spurs itaungana na klabu nyingine za England zinazomilikiwa na matajiri wanaotokea nchini Marekani.
Klabu nyingine zinazomilikiwa na Wamarekani ni Crystal Palace, West Ham, Liverpool, Man United, Arsenal, Aston Villa, Bournemouth, Chelsea, Leeds na Fulham.
Kimataifa Bilionea wa Iran kuinunua Spurs
Bilionea wa Iran kuinunua Spurs
Read also
