London, England
Baada ya kuwapo mjadala kuhusu majaliwa yake katika timu ya Liverpool kutokana na matokeo mabaya ya timu hiyo, kocha Jurgen Klopp amesema kwamba bado yupo kamili na timu hiyo.
Liverpool inashika nafasi ya 10 katika Ligi Kuu England na tangu mwaka huu uanze hawajashinda hata mechi moja hali iliyoibua uvumi kwamba Klopp yuko katika wakati mgumu na yuko mbioni kutimuliwa.
Klopp mwenye umri wa miaka 55 aliachana na timu mbili zilizopita baada ya kuzinoa kwa miaka saba kila moja lakini amekiri kwamba hali anayokutana nayo sasa ni tofauti kabisa ingawa amedai kwamba anapambana kuweka mambo sawa.
“Nina majukumu mengi, mengi mno na nalihitaji jambo hilo na nataka kuweka mambo sawa, nimejitoa katika jambo hilo kwa asilimia 100,” alisema.
“Nina uzoefu wa kutosha kujua kwamba naweza kuondokana na haya kwa sababu ya mambo mawili, nilipoondoka Mainz ilikuwa ni hatua pia katika kazi yangu, nilipoondoka Dortmund (Borrusia) wakati huo nilikuwa nimechoka kweli na nilifikiria ni wakati wa kufanya kitu kingine,” alisema Klopp.
“Kwa sasa bado nipo hapa kwa asilimia 100 lakini naelewa watu wanaposema mambo ya miaka saba lakini hilo halihusiani na lolote, mambo ni magumu hapa kwa sababu nyingine na hili la mwaka si moja ya sababu,” alisema Klopp
.
Klopp ambaye mwaka jana aliongeza mkataba na Liverpool ambao sasa unafikia ukomo mwaka 2026, wiki iliyopita aliwapa wachezaji wake mapumziko ya siku mbili baada ya kuchezea kichapo cha mabao 3-0 mbele ya Wolves.
Leo Jumatatu usiku Liverpool inaumana na mahasimu wao Everton, mechi ambayo itakuwa mtihani mwingine mgumu kwa Klopp ambaye anaamini mazungumzo yake na wachezaji yatawafanya wawe makini na kupata matokeo.
