Manchester, England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola amesema huenda mshambuliaji wake, Erling Haaland akaikosa mechi yao ya keshokutwa Jumatano dhidi ya vinara wa Ligi Kuu England (EPL), Arsenal.
Haaland aliumia na kulazimika kutoka katika mechi ya Man City na Villa iliyopigwa jana Jumapili na Man City kutoka na ushindi wa mabao 3-1.
Kwa mujibu wa Pep mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Norway alilazimika kutolewa wakati wa mapumziko na sasa atafanyiwa vipimo kujua ukubwa wa maumivu ya mguu yanayomkabili.
Ushindi dhidi ya Arsenal unaweza kuifanya Man City iipiku Arsenal kileleni baada ya timu hiyo kuambulia sare ya bao 1-1 katika mechi yao ya juzi Jumamosi dhidi ya Brentford.
Arsenal inashika usukani wa ligi ikiwa na pointi 51 ikifuatiwa na Man City yenye pointi 48 ingawa Arsenal imecheza mechi 21 hadi sasa wakati Man City imecheza mechi 22.
“Erling alipata matatizo na tutaangalia katika siku chache zijazo hali itakuwaje, wakati wa mapumziko nilizungumza na madaktari wakaniambia tusimuweke katika hali hatarishi na nilikubaliana nao,” alisema Pep katika mkutano na wanahabari jana jioni.
“Nafikiri hajaumia sana lakini kesho (Jumatatu-leo) tutaona labda ataweza kucheza Jumatano lakini kama kutakuwa na hali yoyote ya hatari basi hatocheza,” alifafanua Pep..
Pep pia alisema ana mpango wa kuzungumza na wachezaji wake Riyad Mahrez, Rodri na Haaland baada ya wachezaji hao kushindwa kuelewana kuhusu nani aliyetakiwa kupiga penalti katika mechi na Villa.
Haaland anatajwa kuwa ndiye mwenye majukumu ya kupiga penalti lakini Rodri aliingilia kati katika uamuzi wa kumpa mpira Mahrez ambaye hatimaye aliifungia Man City bao la tatu kwa penalti hiyo.
