Tunis, Tunisia
Yanga leo Jumapili imeanza na mguu mbaya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuchapwa mabao 2-0 na US Monastir ya Tunisia katika mechi ya Kundi D.
Mabao yaliyoizamisha Yanga iliyokuwa ugenini yote yalipatikana kipindi cha kwanza yakifungwa kwa kichwa na Mohammed Sagrawi aliyefunga la kwanza na Boubacar Traore aliyefunga la pili.
Baada ya kufunga mabao, Monastir wakishangiliwa na mashabiki wachache, walifanya mashambulizi machache na kutumia muda mwingi kujihami na kuchelewesha muda na hadi mapumziko Yanga waliumiliki mchezo kwa kiasi kikubwa licha ya kuwa nyuma kwa mabao mawili.
Yanga ilikianza kipindi cha pili kwa kushambulia, dakika moja tu baada ya kuanza kipindi hicho, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ alimpenyezea pasi Fiston Mayale ambaye alifumua shuti lakini kipa wa Monastir alikuwa makini na kuokoa mpira huo.
Monastir walijibu shambulizi hilo dakika chache baadaye ambapo Traore akiwa karibu na lango la Yanga aliupiga mpira ambao kama si umahiri wa kipa Djigui Diarra, Monastir wangepata bao la tatu.
Shambulizi hilo lilimsababishia kadi ya njano, Traore ambaye baada ya Diarra kuudaka mpira na kukimbia nao hatua chache ili awapasie wachezaji wake, Traore alimzuia njiani na ndipo mwamuzi alipompa kadi hapo hapo.
Dakika ya 58, Stephan Aziz Ki alipiga mpira wa adhabu ambao kipa wa Monastir aliuokoa na kuangukia ndani ya lango lake kabla ya kulala chini akilalamika kuumia baada ya kuokoa mpira huo.
Baada ya shambulio hilo Yanga waliendelea kuutawala mchezo lakini dakika ya 69, Monastir walifanya shambulizi jingine baada ya Yusuf Omar kuwatoka mabeki wawili wa Yanga lakini mpira alioupiga uliokolewa na Diarra.
Dakika ya 82, Mayele nusura aipatie Yanga bao baada ya kuunganishiwa pasi na Kennedy Musonda lakini shuti alilopiga lilitoka nje.
Katika mechi nyingine ya kundi hilo iliyochezwa leo, TP Mazembe ya DR Congo ilitoka na ushindi wa mabao 3-1 mbele ya Real Bamako ya Mali.
Yanga sasa inajiandaa kucheza mechi yake ya pili ya kundi hilo, Februari 19 ikiwa nyumbani dhidi ya Mazembe wakati Monastir itakuwa ugenini Mali dhidi ya Real Bamako.
Kimataifa Yanga yakwama Tunisia
Yanga yakwama Tunisia
Read also
