Barcelona, Hispania
Rais wa klabu ya Barcelona, Joan Laporta amethibitisha kuwa mtoto wa nyota wa zamani wa timu hiyo, Ronaldinho au Gaucho aitwaye Joao de Assis Moreira anakamilisha taratibu za kujiunga na klabu hiyo.
Mtoto huyo wa Gaucho tayari ameshafanya majaribio katika klabu hiyo ya Nou Camp baada ya kuihama klabu ya Cruzeiro ya kwao Brazil.
Baada ya kuwapo habari zisizo rasmi kwa siku kadhaa kuhusu Joao, Laporta aliwaambia waandishi wa habari jana Alhamisi kwamba mtoto huyo wa Gaucho atabaki Barca.
“Kwa hakika tuna furaha, Ronaldino na kaka yake Roberto wanaifikiria Barca, mtoto wa Ronaldinho anaendelea kucheza soka Barca,” alisema Laporta akimzungumzia Joao ambaye ana miaka 17.
“Alikuwa Cruzeiro, ni kijana mdogo lakini tutampa mkataba kuna mambo machache ya kukamilisha, bado hatujajua kama atakuwa na timu B ya vijana chini ya miaka 19 au la lakini tuna furaha kuwa naye,” alisema Laporta.
“Kuna presha kwa kijana huyu, ni jambo zuri kwa sababu Ronaldinho alikuwa mmoja wa wachezaji bora katika historia, mtoto yuko kwenye presha lakini ni kazi ya makocha wetu kukiendeleza kipaji chake,” aliongeza Laporta.

Mapema wiki hii Ronaldinho alisema kwamba kwa sasa atatumia muda mwingi akiwa Barcelona, mtoto wake yuko katika klabu hiyo na itakuwa vizuri kwake kujua hali yake na anavyoishi Catalunya.