Na mwandishi wetu
Mshambuliaji kinara wa Yanga, Fiston Mayele amesema mazoezi magumu wanayoyafanya tangu wafike nchini Tunisia yatawasaidia kufanya vizuri kwenye mchezo wao wa mkondo wa kwanza wa hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Monastir.
Zimesalia saa 24 kabla ya miamba hiyo ya Tanzania Bara, kushuka katika dimba la Olimpiki Hammadi Agrebi mjini Tunis kucheza mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Akizungumza kupitia mtandao wa klabu hiyo, mshambuliaji huyo ameeleza kuwa tangu wawasili nchini humo wamekuwa wakifanya mazoezi magumu na hiyo ni kutokana na uzito wa mchezo wenyewe na uhitaji wa matokeo wanayoyahitaji katika mchezo huo wa ugenini.
“Siku mbili zilizopita tangu tumefika hapa tumekuwa tukifanya mazoezi mazito hii ni kutokana na ugumu waliokuwa nao wapinzani wetu Monastir, tumekuja huku malengo yetu ikiwa ni kuchukua pointi tatu na kama ikishindikana wapate hata pointi moja,” alisema Mayele.
Mshambuliaji huyo ameeleza kuwa changamoto kubwa wanayopambana nayo nchini humo ni baridi kali lakini anashukuru kadri siku zinavyokwenda yeye na wachezaji wenzake wameendelea kuizoea na anaamini mpaka kufikia siku ya mchezo wataenda nayo sawa.
Mayele ameeleza kuwa anaamini mchezo wa keshokutwa utakuwa mgumu mara mbili ya ule waliocheza dhidi ya Club Africain ambao walishinda na kupata nafasi ya kutinga hatua ya makundi lakini faida waliyokuwa nayo ni kocha wao, Nasreddine Nabi kuwapa mbinu mbadala baada ya kuwaona wapinzani wao katika baadhi ya mechi walizocheza hivi karibuni.
“Tunatarajia kupata upinzani mkali kutoka kwa Monastir ingawa tumepata bahati ya kuona mechi zao kadhaa kwenye video lakini pia kocha aliwahi kuja huku na amewashuhudia wakicheza mechi mbili, tayari ametupa mbinu za kuwakabili naamini hilo litatusaidia kufikia malengo yetu,” alisema Mayele.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Jumapili hii ukitarajiwa kuanza saa 1 jioni kwa saa za Afrika Mashariki ambapo kwa Tunisia itakuwa ni saa 11 jioni.
