Na mwandishi wetu
Yanga imepaa leo Jumanne kuelekea Tunisia kwa ajili ya mechi yao ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Monastir lakini winga wao, Benard Morrison ameachwa kwa kilichoelezwa kuwa anafanyiwa matibabu.
Uongozi wa timu hiyo umeeleza kuwa wamelazimika kumuacha Morrison kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya kina baada ya kuumia hivi karibuni akiwa kwao Ghana.
Imeelezwa kuwa winga huyo machachari asingeweza kutumika vizuri kwenye mechi za hivi karibuni hivyo ameachwa atibiwe kwa ajili ya baadaye na atakuwa nje kwa muda wa miezi miwili.
Rais wa Yanga, Hersi Said amesema leo Jumanne kuwa mchezaji huyo amekuwa hayuko fiti kwa asilimia 100 na kushindwa kutoa huduma ipasavyo kutokana na shida ya majeraha aliyonayo.
Kutokana na hali hiyo, Heris amesema kwamba wameona ni muhimu kumpatia matibabu kwa kipindi hiki ili awasaidie baadaye kwenye wakati mgumu zaidi.
“Saa nyingine anacheza lakini hayuko sawasawa, sasa shida yake imekuwa kubwa kidogo kwa hiyo sasa hivi tumeamua bora apate matibabu ya uhakika kwa sababu kwenye mwezi wa tatu, wa nne itakuwa kipindi kigumu na atahitajika kwa asilimia 100,” alisema Hersi.
“Kwa hiyo maamuzi ya kumtumia wakati huu hayana maana ikiwa hawezi kutupa asilimia 100, tumekubali kwa sasa apate matibabu mazuri ili awe fiti zaidi,” alisema Hersi.
Msafara wa Yanga unaosafiri leo majira ya alasiri kuelekea Dubai, utapumzika hapo kwa siku moja kabla ya kesho kuendelea na safari ya Tunisia kama ilivyoainishwa na Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe.
Katika mchezo wao huo wa kwanza wa hatua ya makundi, Yanga imeondoka na wachezaji 25 na watu tisa wa benchi la ufundi tisa pamoja na kipa Aboutwalib Mshery ambaye anakwenda kufanyiwa upausaji wa goti nchini humo.
Kamwe pia alisema kwamba tayari kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi yupo Tunisia akisubiri wachezaji wake kuelekea mechi hiyo itakayopigwa Februari 12, mwaka huu kwenye Uwanja wa Olympique de Rades.
“Mechi hii kidogo ina mbinu tofauti, Nabi anajua anakwendaje kucheza na mashabiki wanajua mchezo wa ugenini tuna mpango wa kushinda, uwezo tunao na ikishindikana basi tupate alama moja ya ugenini lakini tusipoteze, ndiyo maana tunakwenda tukiwa na maandalizi makubwa kabisa,” alisema Kamwe.
