Na mwandishi wetu
Yanga imeendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC ikiendeleza dhamira yake ya kulitetea taji la ligi hiyo baada ya kuichapa Namungo FC mabao 2-0.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam Jumamosi hii jioni, Yanga ilinufaika kwa mabao ya Dickson Job kipindi cha kwanza na Stephan Aziz Ki mapema kipindi cha pili.
Job alifunga bao hilo akiunganisha kwa kichwa kona iliyochongwa na Djuma Shaaban wakati Aziz Ki aliyatumia makosa ya kipa wa Namungo, Deo Munishi Dida aliyejichanganya wakati wa kuokoa na kujikuta akimpasia mpira Aziz Ki ambaye aliumiliki vizuri kabla ya kufumua shuti lilikokwenda wavuni.
Kwa ushindi huo Yanga sasa inakuwa imefikisha pointi 59 ikiendelea kuwakimbia mahasimu wao Simba wanaoshika nafasi ya pili wakiwa na pointi 53 ikiwa ni tofauti ya pointi zile zile sita.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa Jumamosi hii, Azam ilishindwa kutamba ugenini mbele ya Dodoma Jiji baada ya kulala kwa mabao 2-1.
Azam hata hivyo inaendelea kubaki katika nafasi yake ya tatu ikiwa na pointi 43 wakati Dodoma Jiji inachupa kutoka nafasi ya 12 hadi ya 10 ikiwa imefikisha pointi 24 sawa na Mbeya City lakini zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
Yanga ingeweza kupata bao la tatu kama mshambualiaji wao nyota, Fiston Mayele angetulia na kuwa makini lakini akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga alishindwa kufanya hivyo.
Ligi hiyo itaendelea tena Jumapili hii kwa mechi kati ya Ihefu watakaokuwa wenyeji wa Mbeya City wakati Ruvu Shooting wataikaribisha KMC.
Soka Yanga yajiimarisha kileleni
Yanga yajiimarisha kileleni
Read also
