Manchester, England
Beki wa kati ya Man United, Raphael Varane amesema kwamba uamuzi wake wa kustaafu mapema kuichezea timu ya Taifa ya Ufaransa umetokana na ratiba kuwa ngumu na yenye kumchosha.
Varane ndio kwanza ana miaka 29 na juzi Alhamisi alitangaza kustaafu kuichezea timu hiyo akiwa na rekodi ya kuichezea mechi 93, akishika nafasi ya 13 kati ya wachezaji walioichezea timu hiyo mechi nyingi.
Mwaka 2018 alikuwa na timu ya Ufaransa iliyobeba Kombe la Dunia nchini Urusi na Desemba mwaka jana alikuwamo katika kikosi kilichofikia hatua ya fainali ya michuano hiyo lakini walishindwa kutamba mbele ya Argentina waliobeba kombe hilo.
Baada ya kutangaza kustaafu, Varane alilalamikia ratiba ngumu ya michuano mbalimbali na hivyo ili kujipunguzia mzigo akaamua kustaafu timu ya Taifa.
“Nilijitoa kwa kila kitu, kimwili na kiakili lakini mwishowe unakuwa mfano wa mashine ya kufulia nguo, unacheza kila mara bila kupumzika,” alisema Varane.
“Tuna ratiba iliyobeba michuano mingi na mnacheza bila kupumzika kwa sasa najiona kama mzigo umenizidia,” alisisitiza Varane ambaye alianza kuichezea Ufaransa mara ya kwanza mwaka 2013.
Wakati Varane akistaafu kuichezea timu hiyo akiwa na miaka 29, nahodha na kipa wa timu hiyo, Hugo Lloris yeye alitangaza kustaafu kuichezea timu hiyo mwezi uliopita akiwa na miaka 36.
Tatizo la ratiba ya michuano kuwa ngumu kwa wachezaji liliwahi pia kuzungumzwa na kipa wa Real Madrid, Thibaut Courtois ambaye mwaka 2021 alililalamikia Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) kwa kuwa na ratiba ngumu kwa wachezaji.
Kipa huyo alinukuliwa akisema kwamba wachezaji wanafanywa kama ‘maroboti’ kwa kubebeshwa kalenda ya soka ngumu na yenye mashindano mengi.
