Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba SC, Robert Oliveira ‘Robertinho’ ametua nchini alfajiri ya kuamkia leo Jumatano kuendelea na majukumu yake ikiwemo kuandaa kikosi cha kuivaa Singida Big Stars katika mechi itakayopigwa Ijumaa hii.
Robertinho aliondoka Simba na kurejea kwao Brazil alikodumu kwa takriban wiki moja akielezwa ana shughuli binfsi za kifamilia na kuiacha timu hiyo chini ya kocha msaidizi, Juma Mgunda.
Tangu kuondoka kwa kocha huyo, Simba imecheza mechi moja ya Kombe la FA dhidi ya Coastal Union na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kitu kilichomfurahisha Robertinho akieleza ni suala zuri Simba kuwa na mwendelezo wa ushindi mfululizo.
“Ni vizuri kurejea hapa, nimekuja nikiwa na morali ya mwisho sababu nimeandaa programu nzuri kwa Simba kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu na Kombe la FA lakini la muhimu zaidi kichwani mwangu ni mwendelezo wa ushindi, ikiwemo kucheza kwa ufasaha, kushinda na kuchukua pointi,” alisema Robertinho.
Kocha huyo ametua ikiwa ni siku moja tangu timu hiyo iiingie kambini kujiandaa kuivaa Singida katika mechi ya Ligi Kuu NBC itakayopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Robertinho aliyetua Simba hivi karibuni akitokea Vipers ya Uganda huo utakuwa mchezo wake wa tatu kuiongoza Simba baada ya awali kuibuka na ushindi dhidi ya Mbeya City kwa mabao 3-2 kabla ya kuichapa Dodoma Jiji bao 1-0.
Kocha huyo pia ameiwahi Simba katika kipindi muhimu ikijiandaa na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi itakayoanza Februari 11 mwaka huu dhidi ya Horoya AC, Raja Casablanca na Vipers.