Manchester, England
Manchester United imefanikiwa kumsajili kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu huu, kiungo Marcel Sabitzer kutoka Bayern Munich ya Ujerumani.
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amepigania kumsajili kiungo huyo mwenye miaka 28 akiamini atasaidia kuziba pengo la Christian Eriksen anayeandamwa na majeruhi na Scott McTominay ambaye pia hayuko sawa.
Sabitzer ameichezea Bayern mechi 54 tangu ajiunge nayo, Agosti 2021 alieleza kufurahishwa na usajili huo akisema kwamba kwenye maisha kuna wakati tunalazimika kufanya maamuzi muhimu na ya haraka.
“Mara tu baada ya kusikia fursa hii nilijua ilikuwa sahihi kwangu, mimi ni mchezaji mpambanaji, nataka kushinda na kuisaidia klabu kufanikisha malengo yake msimu huu,” alisema Sabitzer ambaye pia aliwahi kuwa nahodha wa klabu ya RB Leipzig ya Ujerumani siku za nyuma.
“Najiona niko katika kiwango cha juu kama mchezaji na naweza kutoa mchango kwa kiasi kikubwa kupitia uzoefu na nguvu zangu katika kikosi, nina furaha kuanza maisha mapya na wachezaji wenzangu wapya na kocha mpya na kuonyesha uwezo wangu kwa mashabiki wa United.”
Sabitzer pia ameichezea timu ya Taifa ya Austria mara 68 na kufunga mabao 12, anasubiriwa kuibeba United inayoshika nafasi ya nne katika Ligi Kuu England ikiwa nyuma ya vinara Arsenal kwa tofauti ya pointi 11.
Usajili wa mchezaji huyo kwa ujumla unakwenda kuimarisha safu ya kiungo ya kati ambayo kutokana na Eriksen kuwa majeruhi tangu Aprili na kukosekana kwa McTominay, viungo wa eneo hilo waliobaki ni wawili tu, Casemiro na Fred.