London, England
Everton imemtangaza Sean Dyche kuwa kocha mpya akirithi mikoba ya Frank Lampard aliyetimuliwa wiki iliyopita na tayari kocha huyo mpya amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu utakaofikia ukomo Juni 2025.
Lampard ametimuliwa kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo kwenye Ligi Kuu England (EPL) timu hiyo ikiwa nafasi ya 19 na imemchukua Dyche ambaye amekuwa bila kazi tangu Aprili mwaka jana alipotmuliwa na klabu ya Burnley.
Dyche mwenye umri wa miaka 51 anakuwa kocha wa saba katika klabu hiyo tangu Februari 2016 klabu hiyo iliponunuliwa na kibopa Farhad Moshiri.
“Maofisa wangu pamoja nami tuna shauku ya kuisaidia klabu hii kubwa irudi katika ubora wake, najua kuhusu tamaa ya mashabiki wa Everton na vipi klabu hii ina maana kubwa kwao, tuko tayari kufanya kazi na kuwapa kile wanachokitaka,” alisema Moshiri.
Mechi ya kwanza ya Everton katika EPL ikiwa na Dyche itakuwa Februari 4 dhidi ya vinara wa ligi hiyo Arsenal na baada ya hapo watakuwa na kibarua kingine Februari 13 dhidi ya mahasimu wao Liverpool.
Katika kibarua chake Dyche atakuwa akisaidiwa na winga wa zamani wa Nottingham Forest, Ian Woan pamoja na mchezaji wa zamani wa England, Steve Stone.
