London, England
Chelsea imetoa ofa ya Pauni 105 milioni ili kumsajili kiungo wa Benfica na timu ya Taifa ya Argentina, Enzo Fernandez dau ambalo likikamilika litamfanya mchezaji huyo aweke rekodi ya uhamisho.
Hadi sasa bado hakuna uhakika kama ofa hiyo itakubaliwa na ikikubaliwa, itakuwa kubwa kuliko ile ya mwaka 2021 ambapo Man City ilitoa Pauni 100 milioni kumsajili Jack Grealish kutoka Aston Villa.
Fernandez amejipatia umaarufu zaidi wakati wa fainali za Kombe la Dunia akiwa na timu ya Argentina ambayo hatimaye ilibeba taji hilo huku mchezaji huyo akitangazwa kuwa nyota mwenye umri mdogo.
Benfica iliwahi kuituhumu Chelsea kwa kumsumbua kiungo huyo ambapo kocha wake, Roger Schmidt aliwahi kunukuliwa akisema kwamba ‘wameufunga’ mpango wa Chelsea kumsajili mchezaji huyo.
Ni dhahiri kwamba uamuzi wa Chelsea kutangaza dhamira ya kumtaka mchezaji huyo huenda wana uhakika mpango wao unaelekea kufanikiwa.
Fernandez alijiuunga na Benfica akitokea klabu ya River Plate ya Argentina August mwaka jana kwa ada ya Pauni 10 milioni na hadi sasa ameifungia timu hiyo mabao manne katika mechi 29 za Ligi Kuu ya Ureno.
Iwapo usajili wa mchezaji huyo ambaye Januari 17 mwaka huu alifikisha miaka 22, utafanikiwa utaifanya Chelsea kushika nafasi ya kwanza kwa kutumia pesa nyingi za usajili kwa msimu mmoja.
Tangu majira ya kiangazi klabu hiyo imetumia Pauni 270 milioni ikiwa imezidiwa na Real Madrid pekee hadi sasa ambayo mwaka 2019 ilitumia Pauni 292 milioni.
Kimataifa Chelsea yamtangazia ofa kubwa Fernandez
Chelsea yamtangazia ofa kubwa Fernandez
Read also
