Na mwandishi wetu, Dodoma
Jumapili imekuwa siku nzuri na mwanzo mzuri kwa straika mpya wa Simba, Jean Baleke, ameianza kwa kucheza mechi yake ya kwanza akiwa na jezi ya Simba dhidi ya Dodoma Jiji na kufunga bao lake la kwanza, bao pekee na la ushindi kwa timu yake.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Baleke nyota aliyesajiliwa Simba katika usajili wa dirisha dogo akitokea TP Mazembe ya DR Congo alifunga bao hilo katika dakika ya 45.
Bao hilo lililotokana na mpira mrefu wa ‘freekiki’ uliopigwa na kipa wa Simba, Aishi Manula na kumkuta Kibu Dennis ambaye alimtangulizia Baleke aliyeujaza wavuni baada ya kumuwahi kipa wa Dodoma Jiji, Daniel Magore.
Ushindi huo unazidi kuimarisha dhamira ya Simba kuishusha Yanga kileleni kwani tayari imefikisha pointi 50 ikiwa imezidiwa pointi tatu na Yanga lakini Simba imecheza mechi 21 hadi sasa wakati Yanga imecheza mechi 20 na leo Jumatatu inacheza na Ruvu Shooting.
Katika hali ambayo haikutarajiwa Simba ambayo Januari 28 itakuwa na kibarua kigumu kwenye Uwanja wa Mkapa dhidi ya AC Horoya ya Guinea kwenye Ligi ya Mabingwa, katika mechi na Dodoma Jiji iliwapumzisha mastaa wake kadhaa wa kikosi cha kwanza.
Mastaa ambao waliokosekana katika mechi na Dodoma Jiji ni Joash Onyango, Clatous Chama, Muzamir Yassin, Sadio Kanoute, Peter Banda, Pape Sakho na wengineo ambao haikuweza kufahamika mara moja kama ni kwa ajili ya kuwaandaa na mechi dhidi ya Horoya, majeruhi au ni mbinu tu za kocha kubadili timu.
Kwa upande mwingine, Simba pia katika mechi hiyo mbali na Baleke pia ilimtumia nyota wake mpya, Ismael Sawadogo.
Katika mechi nyingine ya Ligi Kuu NBC iliyochezwa Jumapili hii, Mbeya City waliwakaribisha Mtibwa Sugar na kuutumia vyema uwanja wao wa nyumbani kwa kupata ushindi wa bao 1-0.
Mbali na mechi ya Yanga na Ruvu Shooting, mechi nyingine ya ligi hiyo itakayochezwa leo Jumatatu ni kati ya Singida Big Stars watakaokuwa wenyeji wa Azam FC.
Soka Straika mpya Simba aanza na bao
Straika mpya Simba aanza na bao
Read also
