Barcelona, Hispania
Wakati sakata la kumdhalilisha mwanamke kijinsia likiendelea kumtesa beki wa zamani wa Barcelona, Dani Alves, klabu anayoichezea sasa ya Pumas UNAM ya Mexico nayo imetangaza kumfutia mkataba.
Alves ambaye pia amewahi kuwa beki tegemeo wa timu ya Taifa ya Brazil na klabu za PSG na Juventus anatuhumiwa kumdhalilisha mwanamke mmoja waliyekutana katika klabu ya usiku ya mjini Barcelona.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 39 anadaiwa kufanya tukio hilo, Desemba mwaka jana na Ijumaa aliwasili mahakamani kabla ya jaji kuamua kumnyima dhamana.
Katika taarifa yake iliyopatikana kwa njia ya video, Rais wa klabu ya Pumas, Leopoldo Silva alitangaza kwamba klabu yake imeamua inafuta mkataba wa Alves. “Klabu imefikia uamuzi wa kufuta mkataba na Dani Alves kwa sababu ya kilichotokea,” alisema Silva Rais w Pumas katika taarifa hiyo.
“Hii ni taasisi inayohimiza hekima na usawa na tabia za ‘kiprofesheno’ kwa wanamichezo wake wanawake na wanaume, ndani na nje ya uwanja kwa sababu ni wanamichezo mfano wa kuigwa Mexico na duniani kwa ujumla, hatuwezi kuruhusu tabia zozote ambazo zinaharibu falsafa zetu,” alisema Silva.
Alves alilazimika kurudi Hispania akitokea Mexico kwa ajili ya kujibu tuhuma hizo, alifika mwenyewe kwenye kituo cha polisi mjini Barcelona kabla ya kufika mbele ya jaji kwa ajili ya mahojiano.
Waendesha mashtaka walitaka Alves anyimwe dhamana na jaji akakubaliana nao baada ya mwanamke anayedaiwa kufanyiwa udhalilishaji huo kutoa maelezo yake pamoja na shahidi.
Kwa hali ilivyo sasa, Alves atalazimika kuwa mahabusu hadi kesi hiyo itakaposikilizwa katika siku ambayo bado haijatajwa ingawa amekana tuhuma zinazomkabili.
Kesi ya udhalilishaji kijinsia kwa mujibu wa sheria za Hispania inahusishwa katika matukio ya kulazimisha kufanya mapenzi bila ridhaa ikiwamo ubakaji.
