Barcelona, Hispania
Beki wa zamani wa Barcelona na timu ya Taifa ya Brazil, Dani Alves amekamatwa na kuhojiwa na polisi akituhumiwa kumdhalilisha mwanamke kijinsia.
Alves alihojiwa na polisi leo Ijumaa na shauri lake kufikishwa katika mahakama moja ya Barcelona ambapo atahojiwa na majaji ambao baadaye wataamua hatua inayofuata.
Uchunguzi ulianza kufanywa mapema mwezi huu ukihusisha madai kwamba Desemba mwaka jana, Alves alimdhalilisha kijinsia mwanamke mmoja katika klabu moja ya usiku mjini Barcelona. Alves hata hivyo alikana kufanya jambo lolote baya.
Beki huyo aliyesifika kwa kutumia nguvu kwa sasa ana miaka 39 na anaichezea klabu ya UNAM Pumas ya Mexico, alilazimika kusafiri kutoka Mexico hadi Barcelona kwa ajili ya kukabiliana na tuhuma hizo.
Mwanamke mmoja alifikisha mashtaka polisi Januari 2 mwaka huu akidai kwamba Desemba 30 mwaka jana, Alves ‘alimgusa’ katika namna isiyopendeza ndani ya nguo zake bila idhini yake wakati wakiwa katika klabu moja ya usiku ya mjini Barcelona.
Baada ya kufanyiwa hivyo na Alves, mwanamke huyo alitoa taarifa polisi ambao walichukua taarifa ya shahidi ingawa katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni, beki huyo ambaye pia amewahi kuzichezea Juventus na Paris Saint Germain (PSG) alisisitiza kutofanya jambo lolote baya.
“Ningependa kukanusha kila kitu, kwanza nilikuwa pale katika eneo hilo na watu wengi, nikiwa kwenye maraha, kila mtu anafahamu kwamba napenda kucheza, kuwa na furaha lakini bila kuingilia mambo ya watu wengine,” alisema Alves.
“Samahani lakini simfahamu huyu mwanamke ni nani, simjui, sijawahi kuonana naye katika maisha yangu,” alisisitiza Alves.