Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Singida Big Star, Hans Pluijm amesema ushindi walioupata jana dhidi ya Kagera Sugar umewaongezea ari ya kufanya vizuri kwenye mechi zijazo na kumaliza msimu wa Ligi Kuu NBC kwenye nafasi tatu za juu.
Ushindi huo wa bao 1-0 umeifanya Singida kufikisha pointi 40, na kukaa nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo huku Azam inayoshikilia nafasi ya tatu ikiwa na pointi 43, Simba 44 na kinara Yanga pointi 53.
Pluijm raia wa Uholanzi alikiri kuwa mchezo ulikuwa mgumu na wapinzani wao Kagera Sugar walicheza vizuri hasa kipindi cha kwanza lakini walishindwa kutumia vizuri nafasi walizotengeneza.
“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kujituma na kupata ushindi, unajua haukuwa mchezo mwepesi ukizingatia tumetoka kupoteza mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Mlandege kule Zanzibar kwa hiyo wachezaji walikuwa na uchovu lakini nafurahi kupata pointi hizi tatu,” alisema Pluijm.
Kocha huyo ameeleza kuwa mikakati yao kwa sasa ni kuendelea kupambana ili kumaliza ligi kwenye nafasi ya tatu au nne msimu huu ambayo kwao itakuwa ni mafanikio makubwa sababu ndio msimu wao wa kwanza kwenye ligi.
Naye kocha mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amesema kuwa makosa madogo yaliyofanywa na mabeki wake ndiyo yamesababisha wakapoteza mchezo huo lakini amefuraishwa na kiwango ambacho kimeoneshwa na vijana wake.
“Mchezo ulikuwa mzuri, tulicheza kwa nidhamu na kutengeneza nafasi nyingi lakini hatukufanikiwa kuzitumia, ndio mpira tunakubali matokeo na pia nawapongeza Singida kwa ushindi tunarudi kujipanga kwa mechi zijazo,” alisema Maxime.
Kipigo hicho kimeiacha Kagera katika nafasi ya nane kwenye msimamo wakiwa na pointi zao 24 baada ya michezo 20.
