Na mwandishi wetu
Mlandege ya Zanzibar imeibuka kinara wa michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuilaza Singida Big Stars kwa mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa Ijumaa hii jioni kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Singida Big ilikuwa ikipewa nafasi kubwa kubeba taji hilo kwa mara ya kwanza lakini dakika 90 za mchezo zikawa na matokeo tofauti yaliyotosha kulibakisha taji hilo visiwani Zanzibar.
Mlandege inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar ilianza mapema kudhihirisha dhamira ya kulibakisha taji hilo visiwani Zanzibar baada ya kuandika bao dakika ya saba ya mchezo huo lililofungwa na Bashima Saite.
Juhudi za Mlandege zilizaa bao la pili dakika 12 baadaye lililofungwa na Abdulnasir Mohamed wakati bao pekee la Singida Big lilifungwa dakika ya 50 na Kazadi Kasengu, mshambuliaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Ushindi wa Mlandege unahitimisha mbio za michuano hiyo iliyoanza Januari 3 ikishirikisha timu vigogo kwenye Ligi Kuu ya NBC za Azam, Yanga na Simba waliokuwa mabingwa wa michuano iliyopita lakini timu zote hizo zilitolewa na kuziacha Mlandege na Singida Big kuumana katika hatua ya fainali.
Soka Mlandege kinara Mapinduzi Cup
Mlandege kinara Mapinduzi Cup
Read also
