Na mwandishi wetu
Imeelezwa kuwa uongozi wa Yanga umerejea kwenye mazungumzo na kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ baada ya jana Jumatatu kupewa hukumu ya shauri lao kutoka Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF.
Hiyo ni baada ya TFF kueleza kuwa tayari ilishakabidhi uamuzi wa shauri la pande hizo mbili kwa wahusika wenyewe, hivyo wanafahamu kilichoamuliwa.
Wiki iliyopita Yanga ilipeleka malalamiko TFF juu ya mchezaji wake Fei kuvunja mkataba uliobakiza miaka miwili ambapo shauri hilo lilisikilizwa Januari 6 na 9 mwaka huu kabla ya kuelezwa kuwa limemalizika na majibu wanayo wahusika.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe ambaye hakufafanua kama wamepokea au la hukumu hiyo, zaidi alisisitiza kuwa sasa wapo kwenye mawasiliano ya kitaasisi na yanafanyiwa kazi kabla ya kwenda kwa umma.
“Baada ya majibu ya awali ya kamati ambayo waliyatoa kwa umma kupitia chapisho la mtandao wa TFF, kilichofuata pale ni ishu za ndani za kiutendaji kati ya Yanga kuzungumza na mchezaji Fei, nafikiri ndiyo maelekezo yaliyotolewa pale kwa hiyo kinachoendelea sasa ni mazungumzo ya ndani.
“Tukishafikia mahala pazuri kama uongozi tutakuja na kauli ambayo itakuwa inaelezea baada ya tamko letu la kwanza ambapo tulieleza hali ilivyo mpaka kufikia hapa, tutakuja kuwapa wanachama, mashabiki na Watanzania kwa ujumla nini hatma ya sakata lenyewe,” alisema Kamwe.
Alisema kuwa anafahamu kila mmoja sasa anataka kufahamu kilichoamuliwa ni nini lakini akawataka wadau kuwa watulivu katika kipindi hiki na kwamba majibu yatakuja hivi karibuni baada ya mazungumzo ya kina.
“Baada ya kamati kutoa majibu kila mmoja anataka kufahamu upande wa klabu na mchezaji, sasa sisi ni pande mbili lazima tuzungumze kama kamati ilivyoshauri, baada ya hapo tutakuja kutoa taarifa rasmi sasa kwa mashabiki na wanachama wetu nini hatma ya hili,” alisema.
Soka Yanga, Fei Toto kukaa mezani
Yanga, Fei Toto kukaa mezani
Related posts
Read also