London, England
Mambo magumu kwa kocha wa Chelsea, Graham Potter, ushindi mmoja katika mechi saba, kipigo cha jana Jumapili cha 4-0 mbele ya Man City kwenye Kombe la FA kimeongeza majanga yanayoweza kumfanya atimuliwe.
Potter, kocha wa zamani wa Brighton aliyepewa kazi ya kuinoa Chelsea akichukua mikoba ya Thomas Tuchel, anaandamwa na mikosi ya matokeo mabaya ambayo timu hiyo imekuwa ikiyapata huku kukiwa hakuna dalili ya mambo kubadilika.
Katika Ligi Kuu England (EPL), timu hiyo inashika nafasi ya 10 na imetolewa katika michuano yote ya ndani, mashabiki wameanza kumchoka Potter, katika mechi ya jana kuna baadhi walianza kuimba jina la kocha wa zamani Tuchel na tajiri wa zamani wa klabu hiyo, Roman Abramovich.
Potter ambaye alijipatia mafanikio akiwa Brighton kabla ya kuhamia Chelsea miezi minne iliyopita, kwa sasa hatma yake ndani ya Chelsea imeanza kujadiliwa, mjadala umeanzia kwa mashabiki na bila shaka utahamia kwa mabosi wa klabu kabla ya uamuzi mgumu kuchukuliwa.
Akiwa Brighton aliiongoza timu hiyo kushika nafasi ya tisa kwenye EPL msimu uliopita, mafanikio makubwa katika historia ya klabu hiyo na kwa msimu huu hadi anaondoka timu hiyo ilikuwa nafasi ya nne, akiwa ameiongoza katika mechi sita za mwanzo ikishinda nne, sare moja na kupoteza moja.
Ni mafanikio ambayo yaliwavutia wengi kiasi cha baadhi ya wachambuzi kuamini kwamba siku zijazo Potter angeweza kuwa kocha wa timu ya England kwa namna alivyoiongoza Brighton timu yenye bajeti ndogo na haikushangaza alipohamia Chelsea kuchukua mikoba ya Tuchel.
Tuchel hadi anaondoka Chelsea alikuwa na rekodi ya kuipa vikombe vitatu katika kipindi cha miezi 20 lakini msimu huu haukuwa mzuri kwake kwani licha ya klabu hiyo kutumia Pauni 255 milioni katika usajili lakini mwenendo wa timu haukuwa mzuri.
Hadi Tuchel anaondoka Chelsea ilikuwa nafasi ya sita kwenye EPL, haikuwa na matokeo ya kuridhisha na ndipo uamuzi mgumu wa kumuajiri Potter ulipofikiwa lakini naye licha ya kuanza kwa matumaini, taratibu matumaini yameanza kufifia na sasa anaangiliwa tajiri wa klabu hiyo, Todd Boehly atachukua uamuzi gani.
Boehly alihusika kikamilifu kumpa kibarua Potter Chelsea kwa imani kuwa kwa bajeti ndogo ameweza kufanya makubwa na Brighton na hivyo angeweza kufanya makubwa zaidi akiwa na Chelsea kwa bajeti kubwa lakini hali imekuwa tofauti.
Akizungumzia mwenendo mbaya wa timu hiyo ambayo pia inaandamwa na janga la majeruhi, Potter amekiri kwamba matokeo si mazuri.
“Unaweza kujitetea na kutafuta sababu au kusema matokeo si mazuri, majibu yote hayo ni sahihi, lazima tuwe katika ubora na kuwa wamoja kwa sababu ukweli ni kwamba tunapata tabu katika klabu na hili si jambo zuri kwa namna yoyote ile lakini hapo ndipo tulipo kwa sasa,” alisema Potter.
Kwa upande wake, kocha wa Man City, Pep Guardiola amemtaka tajiri wa Chelsea, Boehly kumpa muda Potter katika klabu hiyo.
Matokeo ya mechi za FA jana Jumapili
Bristol City 1-1 Swansea
Derby 3-0 Barnsley
Cardiff 2-2 Leeds
Hartlepool 0-3 Stoke
Norwich 0-1 Blackburn
Stockport 1-2 Walsall
Aston Villa 1-2 Stevenage
Man City 4-0 Chelsea