Na mwandishi wetu, dar
Ishu ya usajili wa kiungo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ imeingia kwenye sarakasi ya aina yake baada ya Yanga kutoa tamko kuwa ni mchezaji wao halali huku mwenyewe akiaga mashabiki akidai amefika ukomo wa kuitumikia klabu hiyo.
Awali, hivi karibuni kuliibuka tetesi za Fei kuhitajika na Azam kabla ya baadaye kuelezwa kuwa ameshakubaliana kujiunga na timu hiyo kabla ya leo asubuhi kuvuja kwa barua inayoonesha Fei amevunja mkataba na Yanga na sasa yuko huru.
Barua hiyo ya Fei kwenda kwa Yanga iliyoandikwa Desemba 22, mwaka huu ilieleza mchakato mzima wa kufuata vifungu na kueleza kuvunja mkataba huo ikiwemo kuilipa Yanga Sh 112,000,000.
Pesa hiyo ni mgawanyo wa Sh 100,000,000 ambalo ni fungu la usajili wa mwaka 2020 mpaka 2024 pamoja na mshahara wa miezi mitatu ili kukamilisha vipengele namba 2.3, 14.7 na 18 vya mkataba wake.
Hata hivyo, leo mchana pia Yanga ikatoa maelezo kwa umma kuwa Fei bado ni mchezaji wao halali kwa mujibu wa kanuni na taratibu za kimkataba na kwamba barua hiyo iliyowafikia Desemba 23 haina misingi ya kuvunja mkataba baina yao.
“Hakuna misingi ya kikanuni wala kisheria kulingana na mkataba wake ambazo zinampa haki mchezaji kusitisha mkataba wake na klabu kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba wa sasa.
“Kanuni na taratibu za Fifa ziko wazi na zimeelezea taratibu zote juu ya jambo la aina hii, kwamba mkataba baina ya mchezaji na klabu hauwezi kuvunjwa na upande mmoja tu bila kujadiliana na upande wa pili wakati msimu wa ligi ukiwa unaendelea.
“Kwa mazingira hayo, barua ya mchezaji ina dhana potofu na haina misingi ya kisheria ya kuvunja mkataba baina ya klabu na mchezaji. Kwa mantiki hiyo, tumemuagiza Feisal, azingatie matakwa ya mkataba wake kama ilivyoelezwa katika mkataba huo,” ilieleza taarifa hiyo.
Aidha, Yanga ilifafanua kuwa inathamini kiwango na mchango wa Fei, ndiyo maana ilishaanza mazungumzo ya kuboresha maslahi na kuongeza muda wa mkataba na wawakilishi wa mchezaji huyo wakiongozwa na mama mzazi wa Fei lakini wakati wanasubiri majibu wakapata barua hiyo ya Fei.
“Hata hivyo, klabu haijapokea majibu mbadala ya mapendekezo ya maboresho kutoka upande wa Feisal na wawakilishi wake, badala yake tumepokea barua inayoelezea kuvunja mkataba kutoka upande wa Feisal ambayo ni kinyume na makubaliano ya mkataba wake wa sasa.
“Klabu tayari imesharejesha fedha kiasi cha Sh 112,000,000 ambazo Feisal aliziweka katika akaunti za klabu. Yanga, inasisitiza kuwa, Feisal Salum ni mchezaji halali ya Yanga na ana mkataba mpaka Mei 30, 2024.”
Muda mfupi baada ya tamko la Yanga, Fei naye akitumia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram akaweka andiko la kawaaga Yanga na mashabiki wake.
“Umekuwa wakati mzuri sana kuichezea klabu ya Yanga, yenye historia kubwa na ya kuvutia nchini na Afrika. Tumekuwa na nyakati nyingi mchanganyiko, tulifurahi pamoja na tulihuzunika pamoja. Nitakumbuka mengi mazuri yaliyotutokea pamoja na nitasahau yote mabaya kwa haraka sana.
“Kila nikiwakumbuka mashabiki wa Wananchi moyo unakua mzito kuwaaga hivyo hivyo kwa wachezaji wenzangu na viongozi pia kwa upendo mlionionesha tukiwa pamoja kwenye shida na raha. Lakini lisilo budi hutendwa au hunenwa kwahiyo leo nasema kwaherini Wananchi.
“lla maisha ndivyo yalivyo mambo huja na kupita na kuna wakati yanajirudia, mpaka wakati mwingine tena, Kwaheri ya kuonana,” ilieleza tamko hilo.
Kizungumkuti hicho kimeibuka ikiwa kesho Jumapili Azam na Yanga zinatarajia kuvaana kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam huku timu hizo zikikimbizana kwenye kilele cha Ligi Kuu NBC. Yanga inaongoza ligi kwa pointi 44 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 38, Azam ni ya tatu kwa pointi 37 baada ya wote kucheza mechi 17.