Na mwandishi wetu
Sare ya bao 1-1 waliyoipata Singida Big Stars dhidi ya Mbeya City jana imetajwa na timu hiyo kuwa ni mafanikio kwao baada ya kukusanya jumla ya pointi nne wakiwa jijini Mbeya.
Kabla ya mechi hiyo, Singida ilicheza dhidi ya Tanzania Prisons na kushinda kwa mabao 2-1 na hivyo kukusanya pointi nne katika timu za jiji hilo na sasa ikijiandaa kuivaa Dodoma Jiji ugenini pia.
Akizungumza na GreenSports, Ofisa Habari wa Singida BS, Hussein Masanza amesema ingawa sare hiyo imewarudisha nyuma kupambana kuwania kumaliza kwenye nafasi za juu zaidi lakini kwa upande mwingine ni mafanikio kwao kwa pointi hizo nne walizovuna.
“Sare si nzuri sana kwetu inatupunguzia pointi hasa ukiangalia ndoto zetu ni kumaliza kwenye nafasi za juu zaidi katika msimamo wa ligi lakini pia ni mafanikio kwa sababu tumeondoka na pointi nne kati ya sita kwa hiyo si haba,” alisema Masanza.
Alisema kuwa bado wanapambana kutimiza ndoto yao na hawatarajii matokeo mabaya kwenye mechi za ngwe hii ya mwisho ya ligi, hivyo ni jukumu la kila anayehusika na timu kuishi na mtazamo huo kwa ajili ya mafanikio ya kikosi kizima mwisho wa msimu.
Mpaka sasa Singida inashikilia nafasi ya nne ikiwa na pointi 31, ikiachwa pointi sita na Azam ambayo inashika nafasi ya tatu kwa pointi 37, Simba ni ya pili kwa pointi 38 na kinara Yanga inamiliki pointi 44 wakati Mbeya City inashikilia nafasi ya 10 na pointi zake 21.
Soka Singida Big yajivunia pointi 4 Mbeya
Singida Big yajivunia pointi 4 Mbeya
Related posts
Read also