Paris, Ufaransa
Hadithi ya Lionel Messi kurejea Barca inaonekana haipo tena baada ya kuibuka habari mpya kwamba mchezaji huyo amekubali kuongeza mkataba wa miaka miwili na klabu yake ya sasa ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa.
Messi ambaye Jumapili iliyopita aliweka historia kwa kutwaa kwa mara ya kwanza Kombe la Dunia akiw ana timu ya Argentina, mkataba wake wa miaka miwili na PSG unafikia ukomo Juni mwakani lakini gazeti moja nchini Ufaransa limeripoti kuwa yuko mbioni kuongeza miaka mingine miwili.
Habari za ndani zinadai kuwa ingawa mchezaji huyo bado hajafanya mazungumzo ya mkataba ikiwamo kuhusu maslahi yake na muda wa mkataba lakini ameshafanya mazungumzo yasiyo rasmi na kuonyesha utayari wa kubaki katika jiji la Paris na kuendelea kuichezea PSG.
Inadaiwa kwamba kabla hata ya fainali za Kombe la Dunia, vigogo wa PSG walikutana na baba yake Messi, Jorge ambapo walimwambia kwamba wanataka mchezaji huyo aendelee kubaki PSG na kutaka kujua mipango yake ili kujiandaa kwa ajili ya msimu ujao na Jorge akawaambia kuwa Messi bado anataka kubaki katika klabu hiyo.
Vigogo hao inadaiwa watafanya mazungumzo ya mwisho na Rais wa PSG, Nasser al-Khelaifi pamoja na mkurugenzi wa michezo, Luis Campos Januari mwakani wakati ambao Messi atakuwa amemaliza mapumziko ya siku 10 baada kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia.
Inadaiwa pia Messi hajapata ofa kwenye klabu nyingine yoyote zaidi ya PSG na hajawahi kuzungumza na Rais wa Barca, Joan Laporta tangu aondoke katika klabu hiyo ingawa kumekuwa na habari kwamba mabosi wa Barca akiwamo Laporta wana hamu ya kuona mchezaji huyo akirudi na kumalizia soka lake katika klabu hiyo ambayo amekuwa nayo muda mrefu na kujipatia mafanikio mengi.
Mwezi uliopita pia ziliwapo habari kwamba klabu ya Inter Miami CF ya Marekani ilikuwa na uhakika wa kumsajili mchezaji huyo mara baada ya fainali za Kombe la Dunia lakini hadi sasa hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa baina ya pande hizo mbili.
Kimataifa Messi anabaki PSG
Messi anabaki PSG
Read also