Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele ametajwa kuwania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka 2022 katika taifa lake la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Katika tuzo hizo zilizoandaiwa na Leopard Leader Foot, nyota huyo atachuana na wachezaji wengine wa taifa hilo wanaokipiga kimataifa kwenye nchi mbalimbali.
Mayele anachuana na Neeskens Kebano kutoka Fulham, Jackson Muleka wa Besiktas, Chancel Mbemba wa Marseille, Yoane Wissa anayekipiga Brentford na Dieumerci Mbokani anayeichezea timu ya Beveren.
Mayele baada ya kutajwa na mtandao huo wa taarifa za soka, aliweka ujumbe kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram na kuomba mashabiki wa soka nchini kumpigia kura ili mwisho wa kinyang’anyiro hicho aibuke kidedea.
“Nimechaguliwa kuwania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa DRC kwa Mwaka 2022, naomba kura yako Mwananchi (shabiki wa Yanga) mwenzangu ili kuniwezesha kushinda tuzo hii”, aliandika
Mchezaji huyo tangu ajiunge na Yanga msimu uliopita akitokea AS Vita amekuwa na mafanikio mazuri kwenye Ligi Kuu NBC, msimu uliopita alishika namba mbili kwa kufumania nyavu mara 16 nyuma ya George Mpole aliyekuwa akikipiga Geita Gold aliyefunga mabao 17.
Ubora wake wa kufumania nyavu uliiongoza Yanga kutwaa mataji matatu msimu uliopita, la Ligi Kuu, Kombe la FA na Ngao ya Jamii ambayo wameitetea tena msimu huu kwa kuifunga Simba mabao 2-1, Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Msimu huu pia, Mayele anaongoza katika orodha ya ufungaji kwa kufunga mabao 11 akikimbizana na mchezaji wa Simba, Moses Phiri raia wa Zambia mwenye mabao 10.