Al-Lusail, Qatar
Argentina imetwaa taji la Dunia ikiibwaga Ufaransa kwa penalti 4-2, haikuwa rahisi, ilikuwa vita kali iliyoongozwa na washambuliaji nyota wa PSG, Kylian Mbappe na Lionel Messi, ilizungumzwa hivyo kabla ya mechi na ndicho kilichoshuhudiwa katika dakika 120.
Wachezaji hao wawili bora kila mmoja akiwa na jezi namba 10, walidhihirisha ni kwa namna gani dunia ilikuwa ikisubiri kuona walivyokuwa wakichuana kuzibeba timu zao za Taifa baada ya mchango mkubwa ambao wamekuwa wakiutoa katika klabu zao na hakika ndicho walichokifanya.




Messi ndiye aliyekuwa wa kwanza dakika ya 23 kumdhihirishia Mbappe kwamba yeye ni zaidi baada ya kufunga bao kwa mkwaju wa penalti, dakika 13 baadaye akapika bao la pili, alimpa pasi Alexis MacAllister ambaye naye alimuunganishia Angel de Maria aliyeipa Argentina bao la pili.
Argentina wakajiona wamemaliza kazi, wakaamua kumpumzisha mchezaji muhimu Di Maria, Mbappe akamjibu Messi dakika ya 80 kwa mkwaju wa penalti, ikawashtua Argentina, dakika moja baadaye akamalizia kazi kwa bao la pili.
Hadi hapo Mbappe akamrudisha Messi na Argentina yake katika dakika 30 za nyongeza, Messi akawa wa kwanza kufunga bao dakika ya 108 lakini Mbappe tena akamalizia kazi kwa bao la tatu la Ufaransa na kufanya matokeo yawe 3-3 huku akijivunia hat trick.
Hatimaye timu zikaingia kwenye mikwaju ya penalti, vita ya Mbappe na Messi ikaanza tena upya, Messi akawa wa kwanza kupiga penalti ya Argentina na Mbappe akawa wa kwanza kwa penalti ya Ufaransa, Messi akafunga na kuwa bao lake la tatu katika mechi hiyo, Mbappe naye akafunga na kuwa bao lake la nne katika mechi hiyo.
Baada ya penalti ya ushindi ya Argentina kupigwa na Gonzalo Montiel kamera ziliwaangaza Messi na Mbappe tena, Messi alikuwa wa kwanza kuanguka chini katikati ya uwanja na kufuatwa na wachezaji wenzake waliolipuka kwa shangwe, upande wa pili ilikuwa sura ya huzuni ya Mbappe, sura iliyoonyesha kutoamini kilichotokea baada ya juhudi kubwa.
Baada ya hapo kamera zikahamia kwenye tuzo, Mbappe na Messi tena wakamulikwa, Mbappe kapanda jukwaani kuchukua Golden Boot, tuzo ya mfungaji bora, Messi naye akapanda jukwaani kuchukua Golden Ball, tuzo ya mchezaji bora wa fainali hizo. Mbappe kamaliza fainali na mabao 12 wakati Messi kamaliza na mabao saba.
Hatimaye Jumapili ya Desemba 18, 22 ikawa siku nzuri kwa Messi na itaendelea kubaki katika kumbukumbu zake kwani ndiye aliibuka shujaa kwa kulibeba Kombe la Dunia 2022 na jezi ya Argentina akimuacha Mbappe katika unyonge.
