Doha, Qatar
Baada ya kuiwezesha Croatia kushika nafasi ya tatu kwenye fainali za Kombe la Dunia, nahodha Luka Modric hana mpango wa kustaafu kwa sasa, badala yake ataendelea kuichezea timu hiyo hadi Juni mwakani kwenye fainali za Europa Nations Ligi.
Modric mwenye miaka 37 sasa, jana Jumamosi aliisaidia Croatia kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Morocco na hivyo kufanikiwa kushika nafasi ya tatu kwenye fainali za Kombe la Dunia zinazofikia tamati leo Jumapili kwa mechi ya fainali kati ya Ufaransa na Argentina.
Alipoulizwa mara baada ya ushindi huo kama atakuwapo kwenye fainali za Ulaya za mwaka 2024 yaani Euro 2024, Modric alisema, “tutaangalia itakavyokuwa, natakiwa kwenda hatua kwa hatua, nafurahia kuwa kwenye timu ya Taifa.”
Modric licha ya umri kuwa mkubwa lakini alianza katika mechi zote saba za Croatia kwenye fainali za Qatar na kucheza kwa dakika 656 na anaamini bado ana nafasi ya kuifanyia mengi nchi yake, “Najiona bado ninaweza kucheza katika kiwango cha juu, nataka kuendelea labda hadi kwenye Nations Ligi, hapo ndipo nitakapopata wasaa wa kufikiria kuhusu Euro 2024,” alisema.

Kitendo cha Croatia kushika nafasi ya tatu kwenye Kombe la Dunia ni mwendelezo wa mafanikio yanayoshangaza wengi ambayo timu hiyo imekuwa ikiyafanya kwenye michuano hiyo kuanzia mwaka 2018 katika fainali za michuano hiyo zilizofanyika nchini Urusi.
Kutokana na umri wa baadhi ya wachezaji huenda wengi wao wasiwemo kwenye timu hiyo katika fainali za Kombe la Dunia za 2026 ingawa kocha wa timu hiyo, Zlatko Dalic amedai kwamba kikosi hicho kina wachezaji wengi chipukizi wa kuziba mapengo hayo.
“Hizi ni fainali za mwisho kwa baadhi ya wachezaji wangu kutokana na umri wao lakini tuna wachezaji wenye umri mdogo katika timu yetu, bado matumaini ni makubwa kwa Croatia, tuna wachezaji wengi chipukizi waliokuwa kwenye benchi, naamini Croatia bado ina mambo mazuri na ya kuvutia kwa miaka ijayo” alisema Dalic.