Na mwandishi wetu
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema wanamshukuru aliyekuwa mtendaji mkuu wao, Barbara Gonzalez aliyeachia ngazi wiki iliyopita kwa kazi kubwa aliyoifanya katika klabu hiyo.
Barbara ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya Vilabu vya CAF na Usimamizi wa Mfumo wa Leseni za Klabu alisema amefanya hivyo ili kutoa fursa kwa viongozi wapya wa klabu watakaochaguliwa Januari mwakani kuchagua mtendaji mkuu na utawala mpya.
Try Again ameeleza kuwa wanamshukuru Barbara kwa kipindi cha miaka miwili aliyokuwa mtendaji Simba kwani licha ya changamoto nyingi alizopitia lakini pia amefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
“Ni kweli mtendaji wetu ameomba kwenda kupata changamoto mpya maana siyo kujiuzulu ni kwenda kupata changamoto mpya, sisi kwenye bodi kwa kweli tunamshukuru kwa kazi kubwa aliyoifanya.
“Kuna mengi mema ameyafanya mazuri kwa klabu yetu lakini kama unavyojua wakati mwingine binadamu anahitaji kubadili changamoto, ameitumikia klabu kwa miaka miwili kwa kazi iliyotukuka, tunamshukuru sana, tunampongeza kwa kazi aliyoifanya, amepita kwenye wakati mgumu lakini amefanikiwa,” alisema Try Again.
Barbara ambaye ameweka rekodi ya kuwa mtendaji mkuu wa kwanza mwanamke kwenye timu za Ligi Kuu nchini, alichukua nafasi hiyo akirithi mikoba ya Senzo Mazingiza raia wa Afrika Kusini aliyehamia Yanga.
Soka Simba wamshukuru Barbara
Simba wamshukuru Barbara
Read also