Na mwandishi wetu
Bondia maarufu, Hassan Mwakinyo ameeleza masikitiko yake juu ya madai ya mabondia wa Zanzibar kuandika barua ya kutomtaka ashiriki kwenye pambano lake linalotarajiwa kufanyika visiwani humo Desemba 30, mwaka huu.
Katika pambano hilo, Mwakinyo anatarajia kupigana na bondia wa nchini Marekani, Peter Dobson kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung kuwania mkanda wa WBC International Super Welter.
Mwakinyo amefafanua hayo leo Jumamosi akieleza bila kutaja mabondia hao wamepeleka barua hiyo kwa nani, lakini kubwa wanapinga ushiriki wa mabondia kutoka Tanzania Bara wakisisitiza hiyo ni fursa ya Wazanzibar pekee.
“Baada ya miaka mingi kupita nimekuwa mstari wa mbele sana kuipambania ‘Boxing ya Zanzibar’ mpaka kufanikiwa kupata ridhaa kupitia Mh. Rais wa Zanzibar na Baraza lake kupata kibali cha kufanya pambano…
“Ajabu ni kwamba mabondia wa Zanzibar wasioona ukubwa wa hili jambo wameandika barua wakidai ile ni fursa yao Wazanzibar na si ya watu wa Tanzania Bara kwa hiyo hawataki tujihusishe nao, sasa sijui ikisemwa kuna muungano uliopo kati yetu, muungano huo unaunganisha kitu gani, hata hivyo kila la kheri mabingwa,” alieleza Mwakinyo kupitia mtandao wa Twitter.
Hilo lilitarajiwa kuwa pambano la kwanza kwa Mwakinyo tangu alipopoteza mara ya mwisho Septemba 3, mwaka huu dhidi ya Liam Smith raia wa England kwenye pambano la ubingwa wa dunia la uzito wa super-welter lililopigwa jijini Liverpool, England.
Ngumi Mabondia Zanzibar wamsikitisha Mwakinyo
Mabondia Zanzibar wamsikitisha Mwakinyo
Read also
