Rio de Janeiro, Brazil
Real Madrid imemsajili mshambuliaji Endrick wa klabu ya Palmeiras ya Brazil. Endrick mwenye miaka 16 amekuwa akitabiriwa na wachambuzi wa soka kuwa mshambuliaji mahiri siku zijazo.
Endrick hata hivyo hatajiunga na klabu hiyo ya Hispania kwa sasa badala yake atafanya hivyo Julai 2024 akiwa amefikisha miaka. Hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa kanuni za Fifa zinazopinga mchezaji chini ya miaka 18 kuhamishwa nchi moja hadi nyingine.
Klabu za Palmeiras na Real Madrid hata hivyo hazijaweka wazi undani wa mkataba wa mchezaji huo kwamba ni wa muda gani badala yake wamesema mchezaji huyo atatembelea makazi ya klabu hiyo mapema wiki ijayo.
Endrick mwenyewe alinukuliwa kupitia mtandao wa klabu ya Palmeiras akisema, “nawashukuru Palmeiras, itabaki kuwa klabu iliyo moyoni mwangu kwa wakati wote kwa kunipa kila kitu muhimu kilichonifanya nifike hapa, kwa kunisaidia kukamilisha ndoto zangu nyingi na kuheshimu shauku yangu na ya familia yangu kuifanya ndoto yangu nyingine iwe kweli.”
“Hadi hapo nitakapojiunga na Real Madrid, kwa sasa nitaendelea kujitolea kwa kila kitu kama ambavyo nimekuwa nikifanya ili kuisaidia zaidi Palmeiras uwanjani,” alisema.
Endrick ambaye kwa sasa anaichezea timu ya taifa ya Brazil ya vijana chini ya miaka 17, kwa msimu huu ameifungia Palmeiras mabao matatu katika mechi saba za ligi ya Serie A ya Brazil.
Rais wa klabu ya Palmeiras, Leila Pereira akizungumzia usajili wa Endrick alisema: “Tumekamilisha mazungumzo makubwa katika historia ya soka la Brazil. Matakwa ya Real Madrid yanaendana na kipaji kikubwa cha Endrick.”
Kimataifa Real Madrid yasajili kinda wa Brazil
Real Madrid yasajili kinda wa Brazil
Read also