Al-Rayyan, Qatar
Staa wa Brazil, Neymar amejikuta akimwaga chozi baada ya Brazil kutolewa na Croatia katika robo fainali ya Kombe la Dunia na kutoa kauli za kukata tamaa akiamini amefika mwisho kwenye michuano hiyo mikubwa ya soka duniani.
Brazil, jana Ijumaa ilitolewa na Croatia kwa penalti 4-2 baada ya sare ya bao 1-1 katika mechi iliyochezwa kwa dakika 120.
“Ukweli ni kwamba sijui, nafikiri kuzungumzia sasa inaweza kuwa jambo baya kwa sababu bado niko katika kipindi cha maumivu, labda sizungumzi moja kwa moja,” alisema Neymar mara baada ya Brazil kutolewa kwenye fainal hizo.
“Kusema kwamba hizi ni fainali za mwisho kwangu inaweza kuwa ni kujiwahisha mimi mwenyewe lakini pia siwezi kuwa na uhakika na lolote, ngoja tuone nini kitatokea huko mbele,” alisema Neymar akiwa katika hali ya unyonge.
“Nataka kutumia muda huu kufikiria hilo, kufikiria nini ninachokitaka mimi mwenyewe, siwezi kufunga mlango wa kuichezea Brazil lakini pia siwezi kusema nina uhakika wa kurudi kuichezea timu hii kwa asilimia 100,” alisema.

Katika mechi hiyo, Neymar hatimaye aliifikia rekodi ya gwiji wa Brazil, Pele aliyekuwa kinara wa mabao kwa timu ya taifa akiwa amefunga mabao 77 baada ya kufunga bao la kwanza lililoibua matumaini ya Brazil kufuzu nusu fainali kabla ya mambo kuharibika.
Neymar alionekana akiwa chini, mnyonge huku akitulizwa na wachezaji wenzake akiwamo mtoto wa mchezaji wa Croatia, Ivan Perisic ambaye alionekana kuwa kivutio kwa namna alivyomsogelea mchezaji huyo wa PSG ya Ufaransa.
Wakati penalti zikiendelea kupigwa, Neymar alitarajiwa kupiga penalti ya tano lakini mambo yalikwenda kombo baada ya Marquinhos kukosa penalti ya Brazil na kuwa neema kwa Croatia ambayo sasa inasubiri kuumana na Argentina katika nusu fainali.