Paris, Ufaransa
Rais wa klabu ya Paris Saint-Germain (PSG), Nasser al-Khelaifi amesema ana uhakika mshambuliaji wao, Lionel Messi atabaki katika timu hiyo na kwa sasa shauku yao ni kumsajili mshambuliaji wa Man United, Marcus Rashford.
Mkataba wa Messi na PSG unafikia ukomo Juni mwakani huku kukiwa na ripoti zinazomhusisha mchezaji huyo na mipango ya kujiunga na klabu ya Miami CF ya Marekani ingawa pia kuna habari kwamba Messi hajakubali mpango wa kwenda Marekani.
Messi ambaye pia ni nahodha wa timu ya Argentina ana nafasi ya kuongeza mwaka mmoja katika mkataba wake na PSG kwa mujibu wa mkataba wake wa sasa na Al Khelaifi amenukuliwa akisema kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 ana raha katika klabu hiyo ya Paris, Ufaransa na atapenda kuendelea kuwa klabuni hapo.
“Ana furaha, unaweza kuliona hilo kwenye timu yake ya taifa, kama mchezaji hana raha utaona kiwango chake hakiwi kizuri kwenye timu ya taifa, amecheza vizuri msimu huu kwa ajili yetu, amefunga mabao mengi na ana asisti nyingi kwenye timu ya taifa na klabu,” alisema Al Khelaifi.
“Kwa hiyo tulichokubaliana pamoja ni kwamba baada ya fainali za Kombe la Dunia tutakaa pamoja, pande zote mbili, upande wetu klabu na yeye sote tuna furaha kwa hiyo tutazungumza baada ya Kombe la Dunia,” alisisitiza bosi huyo wa PSG.

Akimzungumzia Rashford ambaye tayari ameifungia England mabao matatu kwenye fainali za Kombe la Dunia na ambaye mkataba wake na Man United unafikia ukomo Majira ya Kiangazi na hivyo PSG wataweza kumsajili akiwa mchezaji huru.
“Ni mchezaji mwingine wa aina yake na kumpata akiwa huru ni jambo ambalo kila klabu italipenda, hatufichi hilo, tuliwahi kulizungumza hapo kabla na tunavutiwa naye lakini huu si wakati mzuri kwa pande zote mbili labda wakati wa Majira ya Kiangazi, kwa sasa muacheni afikirie Kombe la Dunia na baada ya hapo labda Januari tutazungumza naye tukimhitaji,” alisema Al Khelaifi.