Madrid, Hispania
Baada ya Hispania kutolewa kwenye fainali za Kombe la Dunia katika hatua ya mtoano, kocha wa timu hiyo, Luis Enrique ameachia ngazi.
Enrique mwenye umri wa miaka 52 amekuwa kocha wa timu hiyo tangu mwaka 2018 na kuiongoza Hispania katika kinyang’anyiro cha Euro 2020 na kuifikisha hatua ya nusu fainali kabla ya kushindwa kufurukuta mbele ya Italia.
“Tungependa kumshukuru Luis Enrique na jopo zima la makocha,” ilieleza taarifa ya Shirikisho la Soka Hispania (RFEF) kuhusu Enrique ambaye tayari kocha wa timu ya vijana chini ya miaka 21 ya Hispania, Luis de la Fuente amependekezwa kushika nafasi yake ingawa uteuzi wake utaidhinishwa na bodi ya RFEF itakayokutana Jumatatu.
Hispania ilianza kwa fujo fainali za Kombe la Dunia za Qatar kwa kuibugiza Costa Rica mabao 7-0 katika mechi yake ya kwanza lakini baada ya mechi hiyo iliambulia sare ya bao 1-1 na Ujerumani kabla ya kufungwa na Japan mabao 2-1.
Timu hiyo hata hivyo ilifuzu hatua ya mtoano lakini ilikwama mbele ya Morocco katika hatua hiyo kwa mikwaju ya penalti 3-0 baada ya dakika 120 za sare.
Hispania iliitikisa dunia mwaka 2010 kwa kubeba Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini na kubeba Kombe la Ulaya mwaka 2012.
Kimataifa Kocha Hispania abwaga manyanga
Kocha Hispania abwaga manyanga
Related posts
Read also