
Doha, Qatar
Kocha wa timu ya Taifa ya Morocco, Walid Regragui amesema timu yao ina malengo makubwa na inaruhusiwa kuwa na ndoto za kubeba taji la dunia ikiwa ndiyo inayoshika usukani Kundi F baada ya ushindi dhidi ya Canada.
Morocco jana Alhamisi ilifanikiwa kuichapa Canada mabao 2-1 na kushika usukani wa kundi lake ikiwa imefikisha pointi saba baada ya awali kutoka sare ya 0-0 na Croatia, pamoja na ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Ubelgiji.
Matokeo hayo yamemfanya Regragui kuwa na furaha iliyopitiliza hasa kutokana na kiwango bora cha timu yake na alipoulizwa iwapo timu yake inaweza kufika mbali na kubeba taji la dunia alisema kwamba wamefanikisha azma ya kupigania malengo hayo.
“Tulijiwekea malengo yetu wenyewe, tulitaka tufanye kila liwezekanalo ili kuvuka hatua ya makundi, tuna malengo makubwa, hatuishii hapa lakini tutakuwa ni timu ngumu kufungika, kwa hiyo ni kwanini tusiwe na ndoto ya kubeba taji la Dunia?” alihoji kocha huyo.
“Tunahitaji timu za Afrika kujiwekea malengo, tunakwenda mechi moja baada ya nyingine, hatuendi kwa namna ya kubweteka lakini tukipambana vizuri tutajiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele,” alisema.
Regragui pia alielezea kufurahishwa zaidi na kiwango cha mchezaji wake, Achraf Hakimi ambaye licha ya kuwa na maumivu ya misuli lakini alitoa mchango mkubwa kwa mafanikio ya Morocco ikiwamo kwenye bao la kwanza la timu hiyo lililofungwa na Youssef En-Nesyri. “Angalia Hakimi, alicheza akiwa majeruhi, watu wote Morocco wanatakiwa kumpongeza kila siku,” alisema.
“Napenda pia kuipongeza timu, ni familia, tuko vizuri ni wakati wa kufanya yaliyo mazuri na kizazi hiki, tuna haki ya kuweka historia na leo (jana) tumeweka historia, najivunia kuwa na Morocco, kufanya jambo kubwa kwa nchi yako, inavutia,” alisema.