Doha, Qatar
Wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2022, Qatar wameweka rekodi ya kuwa timu mwenyeji ya kwanza kuaga mapema katika miaka 92 ya historia ya michuano hiyo baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Senegal jana Ijumaa.
Timu hiyo kidogo ilingane na Afrika Kusini kwani zote zimetolewa katika hatua ya makundi lakini tofauti baina ya timu hizo ni kwamba Afrika Kusini walau ilipata ushindi mechi moja na sare moja na hivyo kuchelewesha kuaga kwao mapema.
Qatar waliopewa uenyeji wa michuano hiyo mwaka 2010 na kuzua sintofahamu huku baadhi ya nchi zikipinga, ilianza mechi yake ya kwanza katika Kundi A kwa kulala kwa mabao 2-0 mbele ya Ecuador Jumapili iliyopita na sasa inasubiri kucheza mechi moja ya kukamilisha ratiba dhidi ya Uholanzi na baada ya hapo kuwa watazamaji.
Sare ya bao 1-1 katika mechi nyingine ya kundi hilo kati ya Uholanzi na Ecuador ndiyo inayoifanya timu hiyo kuaga kwani hadi sasa haina pointi hata moja wakati Uholanzi ina pointi nne sawa na Ecuador, Senegal pointi tatu na hivyo mechi za mwisho ndizo zitakazoamua timu mbili zitakazosonga mbele katika kundi hilo kati ya Senegal, Ecuador na Uholanzi.
Afrika Kusini nayo ni timu nyingine mwenyeji iliyotolewa katika hatua ya makundi lakini walau ilipata ushindi na hivyo kuchelewesha safari ya kuziaga fainali hizo mapema tofauti na Qatar ambayo ikiwa na mechi moja mkononi imeshajua kwamba haimo kwenye fainali hizo.
Akizungumzia kutolewa mapema kwa timu yake, kocha wa Qatar, Felix Sanchez alisema, “Kama mlitarajia tufike mbali katika michuano hii, ni kwamba kilichotokea ni cha kukatisha tamaa, lengo letu ni kuwa washindani. Ni lazima tusahau kilichotokea leo (jana) na kuangalia mbele kwenye mechi yetu dhidi ya Uholanzi.”
Kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia, Qatar ilishatabiriwa kuwa mwenyeji ambaye hatotoa ushindani wowote kutokana na nchi hiyo kutokuwa na historia yoyote ya mafanikio kwenye soka la kimataifa ikiwa haina wachezaji wenye vipaji na wanaocheza ligi kubwa za Ulaya
Kimataifa Qatar waaga mapema
Qatar waaga mapema
Related posts
Read also