Doha, Qatar
Nahodha wa timu ya Taifa ya Wales, Gareth Bale amekata tamaa baada ya kukiri kwamba timu yao kufuzu hatua ya mtoano ya fainali za Kombe la Dunia imekuwa ngumu baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 mbele ya Iran.
Wales inayonolewa na kocha, Robert Page hadi sasa ina pointi moja katika mechi mbili na sasa italazimika kuifunga England ili walau kuwa katika nafasi ya kuweza kufuzu hatua ya mtoano jambo ambalo kimsingi ni gumu.
Timu hiyo iliandamwa na mabalaa katika mechi na Iran iliyochezwa jana Ijumaa baada ya kukubali mabao mawili ya dakika za nyongeza yaliyofungwa na Roozbeh Cheshmi na Ramin Rezaeian na kama hiyo haitoshi kipa wa timu hiyo, Wayne Hennessey alijikuta akitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu mshambuliaji wa Iran, Mehdi Taremi
Bale, aliyeonekana kutegemewa na timu hiyo hakuwa na mchango wowote wa maana zaidi ya shuti moja lililoonekana la maana lakini halikuzaa bao, baada ya mechi hiyo alisema hana namna nyingine ya kuizungumzia timu hiyo zaidi ya kukiri kwamba imejiweka pagumu.
“Tulipambana hadi mwisho lakini inakuwa vigumu mnapopungua uwanjani na kubaki wachezaji 10 kwenye fainali za Kombe la Dunia wakati huo huo unacheza dhidi ya timu nzuri, lakini tunatakiwa kuendelea kupambana, kusimama imara haraka, kwa sasa kuna ugumu lakini lazima tujaribu kupambana kuifunga England, ni hivyo tu,” alisema Bale.
Kwa upande wake kocha Page alisema kwamba kiwango ambacho timu hiyo imekionesha katika mechi hiyo kiko mbali mno na malengo waliyojiwekea.
Kwa Iran ushindi huo unakuwa jambo kubwa na la kujivunia baada ya kuchezea kipigo cha mabao 6-2 dhidi ya England katika mechi yao ya kwanza, matokeo yaliyoanza kutoa dalili kwamba timu hiyo ingekuwa kibonde wa kundi lake ambalo pia lina timu ya Marekani.
Matokeo ya mechi za jana za Kombe la Dunia…
Kundi A
Qatar 1-3 Senegal
Uholanzi 1-1 Ecuador
Kundi B
Wales 0-2 Iran
England 0-0 Marekani
Kimataifa Bale aikatia tamaa Wales
Bale aikatia tamaa Wales
Related posts
Read also