Doha, Qatar
Fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea Qatar huenda zikawa za mwisho kwa nyota wa Brazil, Neymar ambaye mbele ya mashabiki wa Brazil bado ana deni kwani bado hajaifanyia makubwa timu hiyo kwenye michuano ya Kombe la Dunia.
Neymar ambaye jioni ya leo timu yake inacheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Serbia ikiwa Kundi G, amewahi kunukuliwa akisema huenda fainali za Qatar zikawa za mwisho kwake kwani fainali zijazo atakuwa na miaka 34 na hivyo uwezekano wa kuwemo kwenye kikosi cha Brazil ni mdogo au haupo na aliwahi kusema haamini kama bado atakuwa na nguvu za kutosha.
Japo umri umekwenda kidogo lakini Neymar wa sasa yuko katika kiwango bora, amedhihirisha hilo kwa namna anavyoibeba klabu ya PSG ya Ufaransa, na kinachosubiriwa na mashabiki wa Brazil ni kuona akiuendeleza moto huo akiwa Qatar na timu yake ya Taifa .
Fainali za Kombe la Dunia 2014 hazikuwa nzuri kwa Neymar wakati huo akiwa dogo wa miaka 22 baada ya kuumia na ingawa Brazil ilifuzu hatua ya nusu fainali lakini ilikutana na kichapo cha aibu cha mabao 7-1 mbele ya Ujerumani ambao waliibuka vinara wa michuano hiyo.
Mwaka 2018 nchini Urusi, Brazil iliaga hatua ya robo fainali ikishindwa kutamba mbele ya Ubelgiji huku Neymar akitajwa kuwa chini ya kiwango, na safari hii kama ilivyo miaka ya nyuma timu hiyo haijawahi kuachwa kutajwa miongoni mwa timu zenye nafasi ya kulibeba taji huku jina la Neymar likichomoza zaidi kwenye midomo ya mashabiki na wachambuzi pengine kuliko wachezaji wengine.
Kwa Neymar fainali hizi ni fursa kwake kuwalipa deni mashabiki wa Brazil na kuwafanya watoke Qatar vifua mbele kama walivyofanya mara ya mwisho kaka zake kina Ronaldo, Ronaldinho, Roberto Carlos, Rivaldo na wengineo waliolibeba taji hilo mwaka 2002.
Neymar anabeba rekodi za mafanikio tangu akiwa Barcelona, timu aliyojiunga nayo akitokea Santos ya kwao Brazil, ameifungia mabao 105 katika mechi 186 kabla ya kuhamia PSG ambapo hadi sasa ana mabao 115 katika mechi 163. Kwa Brazil, Neymar ana mabao 75 akiwa ndiye mshambuliaji mwenye mabao mengi baada ya Pele.
Takwimu zote hizo ni kielelezo cha mchezaji bora na wa hadhi ya juu lakini bado hajawaonyesha Wabrazili hadhi yake hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia na katika fainali za mwaka huu, ndiye anayepewa nafasi kubwa zaidi kuwadhihirishia hilo mashabiki wa Brazil au kuwalipa deni.
Tangu akiwa Santos, Neymar ni mchezaji aliyekuwa akipewa matumaini makubwa na mashabiki na wachambuzi wa soka, akitajwa kuwa staa atakayeiteka dunia ya soka, bahati mbaya matumaini hayo kwa mashabiki wa Brazil wanaona hayajatimia, na wanachotaka sasa ni kuona Qatar inakuwa nafasi ya Neymar kufanya makubwa.
Huu ni mwaka wa 12 kwa Neymar na timu ya Taifa ya Brazil, pamoja na sifa zote anazohusishwa nazo, anachojivunia na timu hiyo ni tuzo ya dhahabu kwenye Michezo ya Olimpiki mwaka 2016, taji la Shirikisho 2013, zaidi ya hayo Neymar hana taji kubwa na timu ya Taifa, bado hajaipa Brazil hadhi ya kuwa timu iliyobeba taji la dunia mara nyingi.
Mwaka 2019, Brazil ilitwaa taji la Copa America lakini Neymar hakuwamo kwenye kikosi hicho kwa sababu ya kuwa majeruhi na ndio maana fainali za Kombe la Dunia za Qatar zinabaki kuwa karata ya mwisho kwa Neymar.
Qatar ni fursa yake ya mwisho kuweka rekodi itakayoendana na hadhi yake ili kesho na keshokutwa atajwe katika orodha ya mastaa wa Brazil waliowahi kubeba Kombe la Dunia, lakini pia ni fursa nzuri kwake kuwalipa deni mashabiki wa Brazil.
Mechi nyingine za leo
Kundi H
Uruguay v Korea Kusini
Ureno v Ghana
Matokeo Kundi G
Switzerland 1-0 Cameroon