Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Simba, Peter Banda atalazimika kukaa nje ya uwanja kwa miezi mitatu kutokana na majeraha aliyonayo ya mguu wa kushoto.
Banda ambaye aliumia wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Sindida Big Stars ambapo alifunga bao katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya 1-1 sasa anatarajia kurejea tena kuitumikia Simba Februari, mwakani.
Banda raia wa Malawi alitoa taarifa za maendeleo yake hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.
“Habari watu wazuri, habari ya leo? Najisikia vizuri sasa kuliko hapo awali. Nitakwenda kuonana na daktari baada ya wiki mbili tena kwa ajili ya uchunguzi lakini kulingana na matokeo, nitakuwa nje kwa miezi mitatu. Natumaini, kwa neema ya Mungu, nitarudi uwanjani mnamo Februari,” aliandika.
Kabla ya kuumia kwenye mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Liti, Singida mnamo Novemba 9, Banda aliisawazishia Simba dakika ya 58 muda mfupi baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Jonas Mkude akimalizia pasi ya Moses Phiri.
Katika mechi hiyo Singida ndiyo iliyotangulia kufunga bao dakika ya 11 kupitia kwa Deus Kaseke aliyemalizia mpira wa krosi uliopigwa na kiungo Said Ndemla.
Soka Banda nje miezi mitatu
Banda nje miezi mitatu
Related posts
Read also