Na Jonathan Haule
Katika Filamu ya Huba juma lililopita tuliona jinsi, Tesa alivyoanza kumgeuka na kuwa mkali kwa Nicole, ambaye kimsingi ni rafiki yake wa ‘dharura’, rafiki aliyekuwa akimtumia ili kuvuruga penzi ya Happy kwa JB, tajiri anayejua kupenda na kutumia pesa.
Tukio la mwisho juma lililopita lilidhihirisha hali hiyo baada ya Tesa kumkoromea Nicole ambaye alifika nyumbani kwake alale ili wakiwa pamoja waangalie namna ya kuyajenga kwa lengo la kumalizia kazi ya kumuondoa Happy kwa JB lakini Tesa akawa amebadilika na kuwa mkali.
Kitendo cha Tesa kumtimua Nicole kinaanza kujibu swali la muda mrefu na la msingi kuhusu urafiki wa wa wawili hawa ambao uliunganiswa na mkakati haramu wa kumtoa Happy kwa JB, mkakati ulioanzia kwa kufanikisha zoezi la kumtorosha Chidi, mume wa Happy kwenye kambi ya shamba la mananasi, ukafuatiwa na mkakati wa kumpeleka Chidi kwa Happy ili Happy aachane na JB.
Yote hayo yamefanyika lakini Happy bado hajatoka kwa JB, je kitendo cha Tesa kumkoromea Nicole na kumfukuza kwake kinaashiria kukata tamaa kwamba mpango umeshafeli na hivyo Nicole hana tena umuhimu kwake au Tesa kashanza kuona dalili za kufanikisha kumtoa Happy na hivyo hahitaji tena ushoga na Nicole.
Yote kwa yote kama ambavyo nimekuwa nikisema mara kadhaa, urafiki wa Nicole na Tesa ni sawa na tukio la dharura, kila mmoja ana ugomvi moyoni mwake dhidi ya mwenzake, kiini cha ugomvi huo ulioko mioyoni mwa kila mmoja wao ni tajiri JB ambaye amewahi kuwaonjesha wote jeuri yake ya pesa kabla ya Happy kuingilia kati na kugeuka adui yao wote.
Swali ambalo pengine linaweza kuanza kupata jibu Jumatatu hii ni hatma ya ushoga wa wawili hawa hasa baada ya mkakati wa kumtoa Happy kwa JB kuonekana kuwa mgumu. Je kila mtu atashika lake au Tesa atabaini kwamba bado anamhitaji Nicole kama ambavyo bado anamhitaji JB.
Tima naye licha ya kuandamwa na jinamizi la huba kati ya Dev na Jude, kabla hajamaliza yake kaamua kuingilia sakata la Happy na Chidi, anaamua kumsaidia Chidi ili waweze kumtoa Happy kwa JB, safari yake kwa JB inafanikiwa baada ya kuingia ndani na kumkuta Happy ambaye bila aibu anamdhihirishia namna alivyonogewa na huba la JB. Kwa alichokishuhudia, Tima anajiaminisha kwamba Happy kwa JB kafika, ni vigumu kutoka kwa ajili ya Chidi.
Hapo hapo mtoto wa pekee wa JB, Nelly naye hafurahii uhusiano wa baba yake na Happy, anaamua kumdhihirishia Happy namna asivyompenda na asivyomkubali kwa kumtolea kauli za dharau, hapo hapo anamtuhumu kwa kuhusika kuondoka kwa Habiba.
Ugomvi wa wawili hawa ni tukio jingine la mfano wa mtoto na ‘mama yake wa kambo’ ambalo linainogesha Filamu ya Huba na kuacha maswali ya je Nelly ataweza kumheshimu Happy ambaye licha ya kuwa ni mpenzi wa baba yake lakini kwake anamuona kuwa ni kero iliyoletwa na baba yake katika nyumba yao.
Roy na Doris nao huba lao limechukua sura mpya, Roy anagundua ushirikina aliofanyiwa na mkwewe Bi Sikitu kwa kuwekwa kwenye chupa, anakuwa mnyonge baada ya kubaini hilo, hapo hapo bado anateswa na kitendo cha mkewe kwenda Pemba bila ruhusa yake. Yote hayo yanaendelea wakati Nandi tayari ana mtoto jambo ambalo halijamfurahisha Doris, mke mwenza wa Nandi.
Nini hatma ya familia hii ambayo nayo imevurugwa na mahaba huku ushirikina ukionekana kupewa nafasi kubwa? Kuanzia Jumatatu hii mengi yatajulikana.
Kibibi, mwanamke mwingine aliyefanikiwa kwa namna ya kipekee kuubeba uhusika wa ujasiri, ukatili na ujeuri katika Filamu ya Huba, anafanikisha mpango wa kumtoa jela Fabrizo, mlinzi na msaidizi wake mwenye kujua siri nyingi za Kibibi na ambaye baadaye uhusiano wao haukuwa mzuri.
Katika tukio hili Kibibi anadhihirisha nguvu ya mwanamke katika huba, anafanikiwa kumpeleka Fabrizo hotelini na kukaa naye pamoja usiku kucha, asubuhi anaamka na kujikagua, jibu analipata kwamba kuna kosa amelifanya, anajuta lakini anaamua kujipa matumaini kwa imani kwamba azma yake ya kumtuliza Fabrizo inaanza kutimia.
Tukio zima la Kibibi na Fabrizo nalo linaacha maswali kwamba nini kitaendelea baina yao hasa kwa kuwa tayari Fabrizo alionyesha kuchukizwa na baadhi ya mambo ya Kibibi, je tayari amelainika na kusahau yote yaliyopita na kuwa mtiifu kwa Kibibi ambaye kuna kila dalili kwamba kumtoa Fabrizo jela hajakufanya hivi hivi tu bali kuna kitu anataka.
Dev, mpenzi wa Kibi naye anahaha kumtuliza Kibibi, anafanya kila analodhani kuwa ni sahihi ili kufanikisha hilo lakini Kibibi bado anaendelea kumfanya kama mtumishi wake wa ndani, anampa hadhi na heshima kwa muda mfupi hasa anapokuwa na matatizo, baada ya hapo anamuonyesha jinsi alivyo katili na jeuri.
Kupotea kwa Carlos nalo ni tukio jingine lenye utata na linaloacha maswali, nini kitamkuta Carlos? ataangamizwa kama walivyofanywa walinzi wengine wa JB na vipi kuhusu JB na mizimu, nani atakayeangamizwa au kutolewa kafara ili awe sadaka kwa mizimu? Majibu yote haya yataanza kupatikana kuanzia Jumatatu hii.
BongoMovie Tesa aanza kumgeuka Nicole
Tesa aanza kumgeuka Nicole
Related posts
Read also