Doha,, Qatar
England imezianza vizuri mbio za fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea Qatar kwa kuibugiza Iran mabao 6-2 katika mechi ya Kundi B iliyochezwa leo Jumatatu.
Iran awali ilipewa matumaini makubwa ya kuonyesha upinzani mkali mbele ya England hasa baada ya timu hiyo kupaa kwa mujibu wa viwango vya Fifa na kushika nafasi ya 20 lakini pia hivi karibuni ilipata ushindi katik mechi yake na Uruguay lakini hali ilikuwa tofauti uwanjani kwani England ilionekana kutawala mchezo kwa kiasi kikubwa.
Jude Bellingham ndiye aliyekuwa wa kwanza kuipatia England bao katika dakika ya 35 akiujaza mpira wavuni kwa kichwa kutokana na krosi ya Luke Shaw kabla Bukayo Saka hajaandika bao la pili katika dakika ya 43 na muda mfupi kabla ya mapumziko, Raheem Sterling aliipatia England bao la tatu akiitumia vizuri krosi ya Harry Kane.
Saka kwa mara nyingine aliipatia England bao la nne katika dakika ya 62, bao ambalo lilionekana kama kuvuruga matumaini ya Iran, matumaini ambayo yalirudi dakika tatu baadaye kwa timu hiyo kupata bao lililofungwa na Mohdi Taremi.
Bao hilo hata hivyo ni kama liliibua hasira za England ambao waliongea bao la tano lililofungwa na Rashford katika dakika ya 71 akiwa ndio kwanza ameingia uwanjani akitokea benchi na Jack Grealish akakamilisha karamu ya mabao ya England kwa kuandika bao la sita katika dakika za lala salama.
Iran hata hivyo mabao hayo hayakuwakatisha tamaa wakaendelea kupambana na Taremi kwa mara nyingine akaipatia timu hiyo bao la pili kwa mkwaju wa penalti ambayo ilitolewa baada ya mchezaji huyo kuchezewa rafu na John Stones.
Katika mechi hiyo, Iran ilipata pigo mapema kwa kipa wake, Alireza Beiranvand kuumia baada ya kugongana kichwani na mchezaji mwenzake wa Iran, Majid Hossein na kipa huyo kuumia kabla ya kutumia muda mwingi kwa matibabu na baadaye ikabainika kwamba asingeweza kuendelea na mchezo.
Kocha wa England, Gareth Southgate mbali na kuipongeza timu yake lakini alisema kwamba walitakiwa kuwa bora zaidi. Nao wawakilishi wa Afrika Senegal walianza vibaya mechi yao baada ya kulala kwa mabao 2-0 mbele ya Uholanzi katika mechi ya Kundi A.
Kimataifa England yaibugiza Iran 6-2, Senegal hoi
England yaibugiza Iran 6-2, Senegal hoi
Related posts
Read also