Na mwandishi wetu
Qatar inapigwa vita isiyo na mantiki kwa kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia, Sepp Blatter, rais wa zamani wa Fifa, mmoja wa watu waliohusika kikamilifu kuipa nchi hiyo uenyeji amegeuka kuwa mshirika wa vita hiyo.
Blatter ambaye Qatar ilipewa uenyeji yeye akiwa msimamizi mkuu wa mchakato huo, hivi karibuni amenukuliwa akisema nchi hiyo haikufaa kuwa mwenyeji, kauli ambayo inaunga mkono kauli nyingi za aina hiyo ambazo zimeendelea kutolewa kila siku.
Miongoni mwa tuhuma ambazo nchi hiyo imekuwa ikihusishwa nazo na kuwa sababu ya kutotakiwa iwe mwenyeji wa michuano hiyo ni unyonyaji na huduma mbaya kwa wahamiaji wanaofanya kazi za vibarua nchini humo, ambao inadaiwa wanaumia na wengine mamia wakidaiwa kufa.
Hoja nyingine ya kupinga uenyeji wa Qatar ni madai kwamba nchini hiyo inakiuka haki za binadamu, haiwapi uhuru wanawake, haithamini na haijali haki za watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja. Zaidi ya hilo Qatar pia inatajwa kuwa ni nchi ndogo, si nchi ya soka na ambayo haina mafanikio makubwa kwenye soka.
Kati ya hoja zote hizo hoja yenye mantiki ni moja tu inayohusu vifo vya vibarua wahamiaji, hoja ambayo hata mamlaka za Qatar zimejaribu kuijibu zikikana kutokea vifo vya mamia ya watu, hoja hii haiwahusu watu wa soka pekee kwa maana ya Fifa bali hata taasisi na mashirika mengine ya kimataifa yote yanatakiwa kuliangalia suala hili na kujiridhisha kama lina ukweli wowote.
Mengine yanayozungumzwa dhidi ya Qatar ni propaganda zilizochelewa na ambazo hazina mantiki, mfano suala la mapenzi ya jinsia moja kupigwa marufuku nchini Qatar ni la kihistoria, lilikuwapo na hapana shaka litaendelea kuwapo miaka na miaka. Siijui katiba ya Qatar lakini sihitaji kuijua ili kujua kwamba mapenzi ya jinsia moja hayana nafasi katika nchi hiyo.
Nchini Qatar iwapo atatokea kiongozi akataka watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja watambuliwe na kuthaminiwa, kiongozi huyo hatopata wa kumuunga mkono na huenda akapewa cheo cha uadui wa taifa.
Ajabu ni kwamba jambo hili linafahamika na kila mtu wakiwamo waliohusika na mchakato wa kuipa nchi hiyo uenyeji wa Kombe la Dunia lakini wakati wa mchakato hawakulizungumza, sasa wakati nchi hiyo imekamilisha kila kitu ndio wanaanza kulizungumza.
Kuna wakati ni muhimu kuheshimu taratibu za nchi na kuacha kushinikiza mambo ambayo yanakwenda kinyume si tu na utamaduni wa kawaida wa kibinadamu bali ambayo hayakubaliki na wananchi walio wengi katika nchi husika.
Hoja kwamba Qatar si nchi ya soka nayo haina mantiki kwani ni nchi yenye ligi ya soka, klabu za soka na mashabiki wengi tu ingawa ligi yake si ya ushindani kama nchi nyingine lakini bado nchi hiyo ni mwanachama wa Fifa hivyo ina haki zote kama wanachama wengine wa Fifa, kama ilivyokuwa na haki Brazil, Urusi, Ujerumani ambazo zimeandaa michuano iliyopita, Qatar nayo ina haki hizo hizo.
Kuinyima nchi hiyo uenyeji kwa sababu hizo ni kufuta dhana nzima ya michuano ya Kombe la Dunia kwamba kila nchi yenye uwezo na mwanachama wa Fifa ina haki ya kuandaa michuano hiyo.
Kombe la Dunia si michuano ya Ulaya, Marekani Kusini au nchi ambazo soka lake lipo juu pekee, ni michuano inayotakiwa kuwa na hadhi ya kidunia miongoni mwa nchi wanachama wa Fifa ikiwamo Qatar na si vinginevyo.
Mashinikizo haya ya dakika za mwisho pia yalitolewa Afrika Kusini ilipokuwa mwenyeji wa michuano hii mwaka 2010, mojawapo ya hoja zilizotolewa ni kuhusu uchumi wa Afrika Kusini na kuishangaa serikali ya nchi hiyo kukubali kutumia fedha ambazo zingeweza kutumika kukabiliana na umasikini, nchi hiyo pia ilitiliwa hofu uwezo wake wa kukabiliana na uhalifu wakati wa fainali hizo.
Mashinikizo yote haya yanatoa picha moja kwamba huenda Qatar ikawa nchi ya mwisho ya Ghuba, kuwa mwenyeji wa michuano hii, kama ambavyo Afrika Kusini inaweza kuwa nchi ya mwisho ya Afrika kuandaa michuano hii. Kinachozungumzwa sasa kinatoa picha kwamba kuna baadhi ya watu wanataka michuano hii ifanyike kwenye nchi tajiri na kubwa.
Kipa na nahodha wa timu ya Ufaransa, Hugo Lloris amekuwa mtu wa kwanza kulalamikia presha dhidi ya wenyeji Qatar akihoji kwamba jambo hilo lilitakiwa kufanywa miaka 10 iliyopita badala ya sasa wakati akili za wachezaji na watu wote tayari zipo kwenye michuano hiyo lakini wanalazimishwa kutolewa kwenye michuano na kujazwa habari za mashinikizo.
Kocha wa Uholanzi, Louis van Gaal, kama ilivyo kwa Blatter naye amepinga nchi hiyo kupewa uenyeji akidai kwamba ni nchi ndogo mno kupewa uenyeji wa michuano mikubwa kama ya Kombe la Dunia lakini walau Van Gaal kawa mkweli kwa kusifu maandalizi na miondombinu ya kuvutia iliyoandaliwa na wenyeji kwa ajili ya fainali hizo.
Alichokisema Van Gaal ndicho kinachopaswa kuangaliwa, ni nchi ndogo kweli tena ina watu wasiozidi milioni tatu lakini imefanya makubwa ambayo nchi nyingine zikiwamo zile ndogo zinapaswa kuiga lakini kwa kinachoendelea sidhani kama nchi zitakazojifunza Qatar zitapata haki ya kuandaa michuano hiyo kwani kuna wakubwa ambao hawataki.
Wakubwa hawa mmoja wao akiwa Blatter wanakataa bila aibu wakati wao ndio waliohusika kuipa nchi hiyo uenyeji wa michuano hiyo.
Kimataifa Qatar inapigwa vita kila kona
Qatar inapigwa vita kila kona
Related posts
Read also