Na mwandishi wetu
Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema siri ya ushindi wa jana Jumatano dhidi ya Namungo ni kazi kubwa iliyofanywa na wachezaji wake ambayo imewawezesha kutimiza lengo lao la kuvuna pointi tatu.
Katika mchezo huo uliopigwa jana Jumatano kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wakifikisha pointi 24.
Kocha huyo ameeleza kuwa lengo kuu katika mechi zao ni kukusanya pointi tatu hivyo kwake ni furaha na kwa sasa akili zao zinafikiria mchezo unaofuata dhidi ya Ruvu Shooting.
“Niwapongeze wachezaji wangu kwa kazi kubwa waliyoifanya, tuliingia kwenye mchezo tukihitaji pointi tatu na Mungu amesaidia vijana wamepambana tumezipata, wapo watu wanahoji kuwa ushindi hafifu lakini hawajui kwamba hii ni ligi na kila timu imejiandaa kupambana,” alisema Mgunda.
Mgunda ameeleza kuwa katika mchezo huo kuna mapungufu ambayo yalijitokeza kwenye safu yake ya ushambuliaji, ameyaona na ameahidi atakwenda kuyafanyia kazi kwenye uwanja wa mazoezi ili kuweka sawa mipango yake.
Aidha kocha huyo amemzungumzia mchezaji Kibu Dennis, kuwa ni mchezaji mpambanaji anayejituma kuipigania timu yake na mapungufu aliyokuwa nayo ni ya kawaida na atamrekebisha kwenye uwanja wa mazoezi.
Naye Kocha Msaidizi wa Namungo, Shadrack Nsajigwa alisema mbinu waliyoingia nayo kwenye mchezo huo ilikuwa ni kuziba njia zote hatarishi ambazo wenyeji wao Simba wanapenda kuzitumia jambo ambalo walifanikiwa kwa kiasi fulani ingawa walipoteza mechi.
“Tulifanya kosa kwenye dakika ya 32 na Simba kupiga mpira nyuma ya mabeki wetu tukajikuta tunaruhusu bao lakini baada ya hapo tuliendelea kulazimisha kupata bao la kusawazisha lakini ilishindikana pia,” alisema Nsajigwa.
Nsajigwa hata hivyo aliwapongeza Simba kwa ushindi huo lakini alisema pamoja na kupoteza mchezo huo wanaridhishwa na timu yao ikiwemo uwezo wa kila mchezaji ndani ya kikosi chao hicho.
Soka Mgunda: Wachezaji wametimiza lengo
Mgunda: Wachezaji wametimiza lengo
Related posts
Read also