Doha, Qatar
Mambo bado magumu kwa mshambuliaji wa Senegal, Sadio Mane ambaye si tu kwamba ataikosa mechi ya kwanza ya fainali za Kombe la Dunia bali huenda akahitaji siku 10 zaidi kabla ya kuwa fiti.
Akizungumzia hali hiyo, kiongozi wa timu hiyo, Abdoulaye Sow alisema kwamba Senegal itakabiliana na hali hiyo licha ya kumkosa mchezaji huyo bora katika mechi yao ya kwanza ya michuano hiyo na wanatakiwa kushinda bila ya Sadio kwa sababu wana wachezaji wengine 25.
“Tutaangalia namna ya kucheza mechi ya kwanza bila ya kuwa na Sadio, hakuna ambaye alitaka hali iwe hivyo lakini hiyo ndiyo hali halisi,” alisema Sow akimzungumzia mchezaji huyo ambaye aliumia chini ya goti la mguu wa kulia.
Sow hata hivyo hakuweka wazi ni mechi ngapi ambazo Mane anatarajia kuzikosa na bado hakujawa na taarifa yoyote kuhusu hilo kutoka Senegal au katika klabu ya Bayern Munich anayoichezea Mane.
Kocha wa Bayern, Julian Nagelsmann hata hivyo Ijumaa iliyopita alitoa kauli ambayo inaonyesha kwamba huenda Senegal isimpate mchezaji huyo alipodai kwamba Mane atahitaji siku zisizopungua 10 kabla ya kufanyiwa vipimo vingine na kujua hali yake.
Mane aliumia wiki iliyopita wakati akiiwakilisha Bayern katika mechi ya Bundesliga dhidi ya Werder Bremen na kutolewa katika dakika ya 20, mechi ambayo Bayern iliibuka na ushindi wa mabao 6-1 na kama kauli ya Nagelsmann ndiyo sahihi basi mchezaji huyo hana nafasi ya kuiwakilisha Senegal iwapo timu hiyo haitafuzu hatua inayofuata.
Sehemu kubwa ya wachezaji wa Senegal wameshawasili Qatar kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia isipokuwa Mane, mechi ya kwanza ya timu hiyo dhidi ya Uholanzi itapigwa Jumatatu wakati Mane bado anasubiri vipimo zaidi kutoka timu ya madaktari wa klabu yake ya Bayern.
Senegal ambao ni mabingwa wa Afrika, baada ya kucheza na Uholanzi, mechi yao ya pili itapigwa dhidi ya Qatar siku nne baadaye kabla ya kukamilisha mechi za makundi Novemba 29 dhidi ya Ecuador.
Kimataifa Mane mambo bado magumu
Mane mambo bado magumu
Related posts
Read also