Na mwandishi wetu
Baada ya kuwapo taarifa kuhusu klabu ya Azam kudaiwa kumuwania kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’, uongozi wa Yanga umeibuka na kusema hawako tayari kumpiga bei mchezaji huyo kwa sasa.
Fei ambaye amekuwa msaada mkubwa tangu ajiunge Yanga msimu wa 2018-19 akitokea JKU ya Zanzibar, ametajwa kuhitajika Azam ambako nako imeelezwa wanaendelea na mikakati ya kukisuka kikosi hicho.
Akizungumzia sual hilo, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe kwanza alikanusha uvumi huo n kuongeza kuwa hawako tayari kumuuza mchezaji huyo na kwa sasa hakuna timu nyingine inayoweza kummiliki Feisal zaidi ya wao wenyewe.
Akisisitiza kuwa hawapo kwenye mlengo wa kumuuza mchezaji huyo, Kamwe alibainisha kwamba hata thamani yake bado hawajaipigia hesabu wakifahamu ni ya juu mno ndiyo maana pia hawajapiga hesabu za Fei kuendelea kukipiga Tanzania akitoka kwao hivi sasa.
“Fei hauzwi, yupo sana wala hawezi kwenda kokote yupo sana hapa Yanga na kama Yanga tutaamua kumuweka sokoni Fei thamani yake bado hatujaijua, hakuna pesa ambayo utaleta sasa na ikaizidi kazi anayofanya Fei, hakuna timu nyingine inaweza kuwa na Fei kwa sasa hapa Tanzania zaidi ya Yanga,” alisema Kamwe.
Ukiachana na Fei kuwa shujaa kwenye sare ya 2-2 dhidi ya Azam msimu huu kwa kuifungia Yanga mabao yote mawili lakini pia kwenye mchezo wa juzi dhidi ya Kagera Sugar, Fei alitoa pasi ya bao pekee lililofungwa na kinda Clement Mziza na hivyo kuendelea kuonesha ubora wake katika msimu mwingine.
Licha ya kucheza kama kiungo mshambuliaji na mara nyingine kiungo wa kati, lakini Fei pia amefanikiwa kufunga mabao manne hadi sasa akizidiwa mawili na mshambuliaji Reliants Lusajo wa Namungo aliyefunga mabao sita.
Soka Yanga: Fei Toto hauzwi
Yanga: Fei Toto hauzwi
Related posts
Read also