Na mwandishi wetu
Kocha Msaidizi wa Namungo FC, Shadrack Nsajigwa, ameitaka klabu ya Simba kujiandaa na kichapo wakati timu hizo zitakapokutana Novemba 16 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Namungo FC, iliyopo nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 15 imedhamiria kumaliza msimu huu kwenye nafasi za juu ili kupata nafasi ya kurudi kushiriki mashindano ya kimataifa.
Nsajigwa, beki wa zamani wa Yanga na Taifa Stars ameeleza kuwa maandalizi wanayofanya ni ya kuhakikisha wanachukua pointi zote tatu mbele ya Simba bila kujali ubora waliokuwa nao Simba.
“Tunakubali Simba ni timu nzuri lakini siyo sababu ya kutufanya tuogope na kushindwa kutimiza wajibu wetu, tupo kwenye maandalizi makali tukijiandaa na mchezo huo na Simba ni timu ambayo inafungika,” alisema Nsajigwa.
Kocha huyo alisema kwamba pamoja na maandalizi wanayofanya lakini wamekuwa wakiangalia marudio ya mchezo wa Simba na Azam FC, ili kuangalia namna Azam walivyofanya hadi kufanikiwa kuifunga Simba.
Alisema kwamba wanachokifanya sasa ni kuwajenga wachezaji wao kwa kuwapa mbinu muhimu na kuwaondolea hofu ili waweze kupambana na kupata kile ambacho wamekikusudia kwenye mchezo huo.
Pamoja na Namungo kuikamia Simba lakini rekodi zinaonesha timu hiyo haijawahi kuifunga Simba wala kupata sare kwenye Uwanja wa Mkapa.
Soka Nsajigwa aitangazia vita Simba
Nsajigwa aitangazia vita Simba
Related posts
Read also