Na mwandishi wetu
Kocha wa Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa anaamini timu yake bado ina nafasi ya kujirekebisha na kufanya vizuri katika michezo ya Ligi Kuu ya NBC iliyobaki ili kujiweka katika mazingira salama.
Kauli ya kocha huyo imekuja baada ya timu hiyo kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wake uliopigwa juzi, ikiwa ni mechi ya tano mfululizo bila ushindi.
Mkwasa ambaye ni kiungo wa zamani wa Yanga, alisema kiwango cha timu yake kinaendelea kuimarika na nafasi waliyopo si nzuri ndiyo maana wanaendelea kupambana huku wakipigania nafasi ya kuwa sehemu nzuri.
“Kila mechi tunayokutana nayo ni ngumu, inaonesha namna gani ligi ni ngumu, kutopata matokeo baadhi ya mechi hakutufanyi tukate tamaa, mapambano yanaendelea, nina imani tutapanda tu nafasi za juu kwa sababu hadi sasa kila mmoja ana nafasi,” alisema.
Ruvu Shooting katika michezo 11 iliyocheza imeshinda mitatu pekee ikipata sare mbili na kupoteza michezo sita, ikishikilia nafasi ya 11 kwa pointi zake 11.
Mkwasa alisema kila mchezo amekuwa akiyaona mapungufu na wanajitahidi kurekebishana ili kutorudia makosa ya mara kwa mara akisisitiza kuwa bado wana nafasi ya kuhakikisha wanapambana kwa uwezo wao wote ili kupata matokeo mazuri na kuondoka katika nafasi za chini walizokaa kwa muda mrefu.
Soka Mkwasa ajipa matumaini
Mkwasa ajipa matumaini
Related posts
Read also