Na mwandishi wetu
Simba na Singida Big Star jioni ya leo Jumatano zimetoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida.
Wenyeji Singida ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 11 lililofungwa na Deus Kaseke ambaye aliiwahi pasi ya Said Ndemla na kuwazidi ujanja mabeki wa Simba kabla ya kupiga shuti lililojaa wavuni na kumpita kipa Beno Kakolanya wa Simba.
Baada ya bao hilo, Simba walianza kasi ya mashambulizi wakitaka kusawazisha lakini juhudi za timu hiyo hazikuzaa matunda ambapo hadi timu zinakwenda mapumziko ni Singida waliokuwa mbele kwa bao hilo moja.
Juhudi za Simba zilizaa matunda dakika 14 baada ya kuanza kipindi cha pili kwa bao lililofungwa na Peter Banda ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Jonas Mkude.
Banda alifunga bao hilo baada ya kuambaa na mpira katika wingi ya kushoto na kufumua shuti ambalo katika hali ya kawaida kwa eneo alilokuwa ilidhaniwa angepiga krosi lakini akaupeleka mpira pembeni kidogo ya mwamba wa lango la Singida na kujaa wavuni kwa mpira huo kumpita kipa Komen Aboubakar ambaye kwa namna alivyojipanga pengine alidhani Banda angepiga krosi.
Azma ya Simba kusaka bao la kusawazisha ilionekana mapema katika kipindi cha pili ambapo katika dakika ya 46 tu, Banda alipiga krosi ya kimo cha mbuzi na Kibu Dennis akajitahidi kuuwahi mpira huo lakini akapishana nao na kama angeugusa kidogo tu ungejaa wavuni.
Dakika za 47 na 48 kwa mara nyingine tena Kibu alishindwa kuipatia Simba mabao akiwa sehemu nzuri, mara ya kwanza shuti lake liliokolewa na kipa Aboubakar na mara ya pili aliiwahi pasi ya juu na kutaka kumpiga kipa kanzu lakini hesabu zikakataa na mpira huo akautoa nje.
Kwa matokeo hayo timu hizo zote sasa zinakuwa zimetoka sare mara tatu tangu kuanza kwa ligi na zote zimefikisha pointi 18 huku Simba ikineemeka kwa wingi wa mabao ya kufunga, ina mabao 18 wakati Singida Big ina mabao tisa, Simba imepoteza mchezo mmoja wakati Dingida Big imepoteza miwili.
Soka Simba, Singida Big hakuna mbabe
Simba, Singida Big hakuna mbabe
Related posts
Read also