London, England
Kocha wa zamani wa Real Madrid na Sevilla, Julen Lopetegui amekabidhiwa jukumu la kuinoa Wolves akirithi mikoba ya Bruno Lage aliyetimuliwa mapema mwezi uliopita.
Julen mwenye umri wa miaka 56 anatarajia kuanza rasmi kibarua hicho Novemba 14 wakati ambao Ligi Kuu England itakuwa imesimama kupisha fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza rasmi kutimua vumbi Novemba 20 mwaka huu.
Awali Julen alitajwa kuanza kazi hiyo mara tu baada ya kutimuliwa kwa Lage lakini hakuwa tayari na badala yake aliamua kukaa nyumbani ili awe karibu na baba yake ambaye umri umeenda.
“Julen ni kocha wa hadhi ya juu, ana uzoefu wa kutosha katika kiwango cha juu kwenye soka,” alisema mwenyekiti wa Wolves, Jeff Shi.
“Tangu mwanzo Julen amekuwa ni chaguo letu la kwanza kwa ajili ya kuinoa Wolves na tunamkaribisha yeye na wasaidizi wake kuungana nasi wiki chache zijazo,” alisema Shi.
Mechi ya kwanza ya Julen kwenye Ligi Kuu England akiwa na Wolves itakuwa ni Desemba 26, ugenini dhidi ya Everton.
Julen alipewa kibarua cha kuinoa Sevilla Juni 2019 na kuiwezesha kutwaa taji la Europa Ligi mwaka 2020 lakini alitimuliwa na timu hiyo, Oktoba mwaka huu baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya katika hatua ya makundi.
Kimataifa Kocha Real Madrid kuinoa Wolves
Kocha Real Madrid kuinoa Wolves
Related posts
Read also