Na mwandishi wetu
Baada ya kuwapo fununu za Yanga kuachana na kocha wao, Nasreddine Nabi, uongozi wa timu hiyo umefunguka rasmi kuwa habari hizo si za kweli na kwamba kocha huyo bado yupo sana Jangwani.
Uwepo wa taarifa hizo uliibuka takriban wiki tatu zilizopita baada ya Yanga kushindwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikitolewa na Al Hilal ya Sudan ikifungwa jumla ya mabao 2-1 na kudondokea Kombe la Shirikisho Afrika.
Taarifa hizo ziliibuka upya baada ya kumalizika kwa mechi yao dhidi ya Simba iliyoisha kwa sare ya bao 1-1, iliyopigwa wikiendi iliyopita Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe leo Jumatano ametoa ufafanuzi kuhusiana na tuhuma hizo akieleza kuwa hawana mpango wa kuachana na kocha huyo, akikanusha pia kukaa kikao na kujadili hatma yake hivi karibuni.
“Taarifa rasmi na msimamo wa Yanga kuanzia rais, makamu wa rais, wajumbe wa kamati ya utendaji, mashabiki na wanachama wa Yanga ni kwamba kocha Nabi ni kocha wa Yanga, bado yupo sana na ataendelea kudumu kwenye klabu hii kwa muda ambao wake unaonesha kwenye makaratasi yetu.
“Kwa hiyo zile presha, zile fununu, zile tetesi ambazo zilitembea sana jana (juzi), tunajua zimeanzia wapi na tunajua ni kwa kiasi gani wanaumia kwamba Nabi amesalia na yupo ana furaha kuwepo hapa, ni watu ambao furaha yao ni kusikia Nabi anaondoka kwa sababu uwepo wake unawapa shida watu na wakisikia anaondoka, wanajisikia vizuri,” alisema Kamwe.
Kamwe alisema si tu wanakanusha uwepo wa taarifa hizo bali hawajahi kujadili suala kama la kumuondoa Nabi, akisisitiza hawajalifikiria kulifanya hilo hata katika siku za usoni kutokana na kuiamini kazi ya kocha huyo raia wa Tunisia.
Nabi alitua kuinoa Yanga katikati ya msimu wa 2020/21 na msimu uliofuata aliisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu NBC, Kombe la FA na kutwaa mara mbili mfululizo Ngao ya Jamii huku sasa akiwa na kibarua cha kuipelekea hatua ya makundi YA Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuumana na Club Africain ya Tunisia.
Soka Nabi bado yupo sana Yanga
Nabi bado yupo sana Yanga
Related posts
Read also