London, England
Nahodha wa timu ya Taifa ya Senegal, Kalidou Koulibaly amesema timu hiyo maarufu Simba wa Teranga inataka kuwa timu ya kwanza ya Afrika kubeba Kombe la Dunia.
Fainali za Kombe la Dunia zitaanza kutimua vumbi Novemba 20 mwaka huu nchini Qatar ambapo katika historia ya fainali hizo hakuna timu ya Afrika iliyofikia hatua ya nusu fainali, mafanikio pekee ni kwa timu hizo kuishia hatua ya robo fainali.
Timu pekee za Afrika ndizo zilizoweka rekodi ya kufikia hatua ya robo fainali ni Cameroon mwaka 2010, Senegal mwaka 2002 pamoja na Ghana ambayo ilipambana mwaka 2010 na kuibua matumaini lakini nayo iliishia hatua hiyo hiyo.
Katika fainali za mwaka huu, wenyeji Qatar watafungua dimba katika mechi ya Kundi A dhidi ya Ecuador wakati siku inayofuata Senegal watajitupa uwanjani katika mechi yao ya kwanza ya kundi hilo hilo dhidi ya Uholanzi.
Koulibaly ambaye ametokea kuwa mchezaji muhimu wa Chelsea kwenye Ligi Kuu England anaamini wawakilishi wa Afrika wanatakiwa kufikiria makubwa na si hatua ya mtoano pekee.
“Mataifa ya Africa yanakosa hali ya kujiamini na umakini kwamba wanaweza kushinda taji la Dunia,” alisema beki huyo wa Chelsea.
“Tunachukulia kwenda mbele ni kuvuka hatua ya makundi ni jambo zuri lakini ni lazima tuweke malengo makubwa sisi wenyewe, sidhani kama timu za Ufaransa au England zinafurahia kutolewe katika hatua ya makundi, wanataka kwenda mbele zaidi, na sisi tunatakiwa kuwa na mtazamo huo, hicho ndicho ninachotaka kwenda nacho Senegal,” alisema.
“Nafikiri huu ni wakati kwa nchi ya Afrika kufanya makubwa na kushinda Kombe la Dunia, kwa sababu ni bara la watu wenye vipaji, tuna wachezaji wakubwa,” alisema.
Februari mwaka huu, Senegal ilitwaa Kombe la Mataifa ya Afrika na kwa sasa nchi hiyo inashika nafasi ya 18 duniani kwa mujibu wa viwango vya Fifa na inakwenda kushiriki fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar ikiwa nafasi ya kwanza kwa nchi za Afrika tangu mwaka 2018.
Wawakilishi wengine wa Afrika katika fainali za Kombe la Dunia ni Cameroon, Ghana, Morocco na Tunisia.
Kimataifa Senegal yapania kubeba Kombe la Dunia
Senegal yapania kubeba Kombe la Dunia
Related posts
Read also