Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa Real Madrid na timu ya Taifa ya Ufaransa, Karim Benzema ametwaa tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka ya Ballon d’Or wakati Alexia Putellas wa Barcelona akibeba tuzo hiyo kwa upande wa wanawake.
Benzema alikabidhiwa tuzo hiyo jana Jumatau usiku na nyota wa zamani wa Ufaransa Zinedine Zidane, akijivunia rekodi ya kufunga mabao 44 katika mechi 46 na kuisaidia timu yake ya Real Madrid kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na lile la La Liga kwa msimu wa 2021-22.
Kwa kipindi cha miaka 12 kati ya 13 iliyopita tuzo hiyo imekuwa ikitawaliwa na wachezaji mastaa wawili ambao ni Lionel Messi wakati huo akiwa Barcelona (sasa anaichezea PSG) aliyeibeba mara saba na Cristiano Ronaldo aliyeibeba mara tano.
Mshambuliaji wa zamani wa Liverpool ambaye kwa sasa anaichezea Bayern Munich, Sadio Mane ameshika nafasi ya pili wakati nafasi ya tatu imekwenda kwa Kevin de Bruyne wa Manchester City
Kwa upande wa wanawake wakati Alexia akiibuka kinara nafasi ya pili imekwenda kwa mshambuliaji wa Arsenal, Beth Mead ambaye pia alikuwamo kwenye timu ya Taifa ya Wanawake ya England iliyobeba taji la Euro 2022.
Hiyo ni mara ya kwanza kwa Benzema kutwaa tuzo hiyo wakati kwa Alexia anakuwa ameitetea baada ya kufanya hivyo msimu uliopita lakini Benzema pia anakuwa Mfaransa wa pili kufanya hivyo tangu alipoibeba Zidane mwaka 1998. Zidane maarufu Zizou pia aliwahi kuwa mchezaji na baadaye kocha wa Real Madrid.
Klabu ya Manchester City ambao ndio vinara wa Ligi Kuu England msimu wa 2021-22, wametwaa tuzo ya klabu bora ya mwaka wakiibwaga Liverpool, washindani wao katika mbio za kulisaka taji la ligi hiyo msimu wa 2021-22.

“Tuzo hii iliyo mbele yangu hakika inanipa cha kujivunia, nilipokuwa mdogo hii ilikuwa ndoto yangu, sikukata tamaa, kila kitu kinawezekana, najivunia safari yangu hadi hapa, haikuwa rahisi, ilikuwa kipindi kigumu kwangu na kwa familia yangu pia,” alisema Benzema ambaye ndiye aliyepewa nafasi kubwa ya kubeba tuzo hiyo ambayo washindi hupigiwa kura na waandishi wa michezo 100 duniani kote.
Benzema ambaye amekuwa na Real Madrid tangu mwaka 2009, anatarajia kuiongoza Ufaransa katika kinyang’anyiro cha fainali za Kombe la Dunia Novemba mwaka huu nchini Qatar.
Washindi wengine wa tuzo hiyo ni kipa wa Real Madrid, Thibaut Courtois aliyetwaa tuzo ya kipa bora wakati straika wa zamani wa Bayern Munich ambaye kwa sasa anaichezea Barcelona, Robert Lewandowski au Lewa ametwaa tuzo ya mshambuliaji bora na tuzo ya mchezaji bora wa umri chini ya miaka 21 imebebwa na kiungo wa Barcelona, Gavi ambaye Agosti mwaka huu alitimiza miaka 18.
Orodha ya wachezaji wa kwanza hadi wa 20 wa Ballon d’Or ni kama ifuatavyo…
- Karim Benzema (Real Madrid)
- Sadio Mane (Bayern Munich)
- Kevin de Bruyne (Man City)
- Robert Lewandowski (Barcelona)
- Mohamed Salah (Liverpool)
- Kylian Mbappe (PSG)
- Thibaut Courtois (Real Madrid)
- Vinicius Junior (Real Madrid)
- Luka Modric (Real Madrid)
- Erling Haaland (Man City)
- Son Heung-min (Tottenham)
- Riyad Mahrez (Man City)
- Sebastien Haller (Borussia Dortmund)
- Fabinho (Liverpool)- Rafael Leao (AC Milan)
- Virgil van Dijk (Liverpool)
- Luis Diaz (Liverpool)-Dusan Vlahovic (Juventus)-Casemiro (Man United)
- Cristiano Ronaldo (Man United)